MAPYA yameibuka siku nne baada ya kutekwa kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, chama hicho kikidai kuwa kiongozi huyo amekutwa na kiwango kikubwa cha sumu mwilini.
Aidha, madaktari wanaendelea kufanya uchunguzi wa kitabibu ili kubaini aina ya sumu hiyo.
Katibu wa Habari na Uenezi wa ngome ya vijana wa chama hicho, Philibert Macheyeki, alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, kuwa mbali na sumu, madaktari wamemfanyia upasuaji mdogo kwenye unyayo.
“Madaktari wamedai mwili wa Abdul Nondo unaonesha kuwa na kiwango kikubwa cha sumu, ambayo mpaka sasa hawajajua kama zimetokana na athari za kupigwa na kuteswa au kama alipewa kitu chenye sumu na watekaji wake,” alisema katika taarifa hiyo.
“Uongozi wa ACT-Wazalendo Taifa, umewaomba madaktari kumfanyia uchunguzi zaidi kwa ajili ya kubaini aina ya sumu iliyo mwilini mwake na kama zimetokana na kupewa sumu kwa sasa hali yake bado sio nzuri, mikono yake imevimba na ana maumivu makali mwilini japo madaktari wanaendelea kupambana kuhakikisha afya yake inaimarika na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.”
Macheyeki alisema Nondo alifanyiwa upasuaji wa unyayo juzi Desemba 3, 2024 baada ya madaktari wa Hospitali ya Aga Khan, alikolazwa kubaini uwepo wa mivunjiko midogomidogo.
Alisema tatizo hilo limesababishwa na kipigo alichofanyiwa na watekaji ambao walimtupa katika ufukwe wa Coco Beach, Dar es Salaam.
Nondo anadaiwa kutekwa Desemba Mosi, mwaka huu kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli, wilayani Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam, akitokea Kigoma alikoendesha kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alidai alichukuliwa kwa nguvu na watu sita, ambao walimfunga mikono na miguu na kumfunika uso kwa kitambaa cheusi na baadaye kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED