Madereva bodaboda 72 mbaroni tuhuma uhalifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:25 PM Mar 27 2024
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP), Almachius Mchunguzi.
PICHA: MALUNDE BLOG
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP), Almachius Mchunguzi.

JESHI la Polisi mkoani Tanga, limekamata pikipiki 72 kutokana na makosa mbalimbali, ikiwemo kujihusisha na uhalifu.

Kwenye idadi hiyo pia wapo waliokamatwa wakijihusisha na makosa mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na namba za usajili, kung’oa bomba la kutolea moshi, kutokuwa na leseni na kutovaa kofia ngumu.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi (ACP), Almachius Mchunguzi,  amesema waendesha pikipiki hao maarufu kama bodaboda, walikamatwa wakati wa operesheni za kukabiliana na wahalifu.

Amesema baada ya upelelezi kukamilika tayari majalada yao yamepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi.

Kamanda Mchunguzi amesema: “Baadhi ya wahalifu hususani watumiaji wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wamekuwa wakifahamika lakini wananchi hawatoi ushirikiano kwa kutosha kufanikisha kuwakamata na kuwafikisha mahakamani”.