MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameweka msimamo kuhusu wabunge 19 wa Viti Maalum, akiwamo Halima Mdee, kwamba hatima yao inategemea mkutano mkuu wa chama hicho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Lissu alisema ili wabunge hao ambao walifutiwa uanachama mwaka 2022 warejee CHADEMA, inabidi kuitisha kikao cha mkutano mkuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.9 ya Katiba ya CHADEMA, Mkutano Mkuu unafanyika kila baada ya miaka mitano. Kwa mantiki hiyo, Mkutano Mkuu wa chama hicho utafanyika mwaka 2030 kwa kuwa ulimalizika Januari 22, 2025 wakati wa uchaguzi wa viongozi wakuu na waandamizi wa chama hicho.
Alisema kama wabunge hao wana dhamira ya kurudi kwenye chama hicho, wanapaswa kujiandaa kujieleza namna walivyoingia bungeni bila idhini ya Katibu Mkuu wa chama.
"Hawajawahi kusema hizo fomu za kugombea nani aliyewapa na kuzisaini wakati zinapaswa kusainiwa na Katibu Mkuu pekee, na John Mnyika hakuwahi kuzitia saini,” alisema.
Alisema baadhi ya wabunge hao walitokea gerezani na kuibukia bungeni, na kwamba chama kitahitaji kujua aliyewapelekea fomu gerezani.
“Kwa hiyo kama wanakuja kutaka suluhu na chama, waje wafungue siri za mioyo yao. Waje na mioyo myeupe na tuichunguze ni myeupe kweli. Wasije tu kwa sababu uchaguzi umekaribia kutaka ubunge,” alisema.
Mbali na Mdee, wabunge waliofukuzwa ni Ester Bulaya, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Jesca Kishoa, Sophia Mwakagenda, Grace Tendega, Conchesta Rwamlaza, Nusrat Hanje na Taunza Malapo.
Kamati Kuu ya CHADEMA iliwafukuza Mdee na wenzake kwa utovu wa nidhamu kwa kosa la kuapishwa kuwa wabunge bila ruhusa ya chama chao.
Baadaye Mkutano Mkuu wa chama hicho ulibariki uamuzi huo jambo lililowafanya wakimbilie mahakamani kulinda ubunge wao.
Hata hivyo, baada ya mvutano mahakamani, CHADEMA kilishinda lakini hadi sasa wabunge hao bado wako bungeni.
Kuhusu ukomo wa viti maalum ya udiwani na ubunge kwa chama hicho, Lissu alisema mabadiliko ya katiba ya CHADEMA pamoja na kanuni, yataweka ukomo wa miaka mitano na baada ya hapo watapaswa kugombea kwenye majimbo.
Katika hatua nyingine, ushindi wa Lissu siku ya Jumanne umevuta hisia za mashabiki wa chama hicho, huku mawakili 11 wakijiunga CHADEMA.
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, aliiambia Nipashe jana kwamba kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi wa kada mbalimbali kujiunga, huku hamasa kubwa ikifanyika mitandaoni.
“Tumeona mwamko mkubwa sana kwenye mitandao ya kijamii watu kutaka kujiunga na chama, siwezi kusema wamejiunga kwa kiwango gani, ni hadi tukusanye takwimu kutoka maeneo mbalimbali,” alisema.
Mmoja wa mawakili waliojiunga na CHADEMA, Matojo Kosatta, alisema wasomi hao wamejiunga kwa kuwa wanaamini chama hicho kinaweza kupigania maslahi mapana ya Watanzania.
“Ni kweli tumejiunga na kuna mawakili wengine watajiunga awamu ya pili. Tunaamini Mwenyekiti wetu (Tundu Lissu), atakipeleka chama katika mwelekeo mzuri. Yale mambo ambayo tulikuwa tunataka yafanyike tunaamini yatafanyika kwa sababu tulikuwa tunatoa ushauri, lakini ukawa haufanyiwi kazi,” alisema.
Kosatta alisema mara kadhaa, baadhi ya mawakili akiwamo yeye wamekuwa wakitoa ushauri wa namna chama hicho kitaweza kujitegemea kimapato na kushinda kwenye uchaguzi, lakini ushauri huo haukuwa unafanyiwa kazi.
“Tulikuwa tunashauri na vitu havifanyiwi kazi kwa sababu kuna watu walikuwa wananufaika kwa CHADEMA kukosa fedha kwa mfano.
“Tunajua Lissu hana maslahi ya kifedha ndani ya CHADEMA, tunajua maslahi yake ni kujenga chama na kuleta ukombozi kwa Watanzania. Lissu anamaanisha anachokisema na tunaona kutakuwa na mabadiliko makubwa ndio maana tumejiunga na tuko tayari kujitolea," alisema.
Alisema anaamini kwamba chini ya Lissu, imani na ari ya wanachama, mashabiki na Watanzania kwa chama hicho itaongezeka.
“Sina mpango wa kugombea nafasi ya siasa kwenye uchaguzi mkuu ujao na nimeongea na baadhi ya wenzangu ambao tumejiunga pamoja kwamba tukakisaidie chama, tukawe rasilimali za kukijenga chama chetu,” alisema Kasotta.
Alisema ili CHADEMA ifanikiwe, lazima kifanyekazi kama timu ya mpira wa miguu, kwa kupanga safu ya walinzi, washambuliaji, wafungaji na golikipa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED