Dk. Jafo: Uboreshaji huduma ya maji Kisarawe kutakuza uchumi

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 07:49 PM Aug 21 2024
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.
Picha: Beatrice Shayo
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo amesema kuboreshwa kwa huduma za Maji, Usafi na Usafi wa Mazingira (WASH) katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani kutakuza ukuaji wa uchumi kutokana na kupungua kwa magonjwa yatokanayo na maji.

Jafo aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya mradi wa uboreshaji wa tabia za usafi kwenye shule 30 na vituo vya afya 15 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh bilioni 4 umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Shirika la WaterAid.

“Upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira unapunguza matukio ya magonjwa yatokanayo na maji kama vile kuhara. Hii inasababisha kupungua kwa gharama za huduma za afya, utoro mdogo wa kazi na shule pamoja na kuhakikisha watu wanakuwa na afya bora,” amesema Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe.

Aliongeza kuwa kuboreshwa kwa huduma za WASH huleta mabadiliko hasa katika masuala ya usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi, hivyo kuikinga jamii na magonjwa yatokanayo na hali duni ya usafi.

1

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga, amesema kwa ufadhili JICA waliweza kubuni mradi wa kufundisha namna bora ya matumizi ya maji katika vituo vya afya 15 na shule 30 katika Wilaya ya Kisarawe.

Amesema mradi huo wameufanya katika kipindi cha miaka mitatu wamepata ushirikiano kutoka serikali na wadau wa maendeleo ambao wamesaidi kufanikisha utafiti huo.

“Utafiti umeonyesha upatikanaji wa maji, usafi wa mazingira na namna endelevu za kufundisha njia bora ya kutumia vyoo na maji katika kunawa kuna uwezekano wa kupunguza magonjwa ambayo yanaambukiza kutokana na uchafu,”amesema.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amesema Wilaya yake bado inahitaji vifaa zaidi vya WASH kwa kuwa ina jumla ya shule 120.

“Ninaomba WaterAid itusaidie katika shule 20 bado tunahitaji huu mradi hasa kwa mabinti wetu wa Kisarawe kwa kuzingatia Wilaya hii yenye matukio mengi ya ukatili wa kijinsia na wengine kuwa ni ‘Masingle mother’ kutokana na mabinti kupewa ujauzito katika umri wa kuanzia miaka 11,”amesema Magoti.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.