TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imemfanyia upasuaji mtoto mchanga wa siku tatu, ambaye mishipa yake ya moyo haikuwa katika mpangilio sahihi.
Upasuaji huo umefanyika katika kambi maalumu ikifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI na wenzao wa kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia.
Kambi hiyo imetoa huduma kwa watoto 23, akiwamo mtoto huyo, ambao wana matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo na kufikisha idadi ya watoto 40 waliopatiwa huduma hiyo tangu kuanza kwa kambi hiyo.
Mkurugenzi wa Upasuaji na Biingwa wa Usingizi na Wagonjwa Mahututi kutoka JKCI, Dk. Angela Muhozya, amesema kambi hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.
“Tangu kambi hii imeanza na tumeweza kuwafanyia upasuaji watoto wapatao 23 na tunatarajia kuwafanyia watoto 40 na kwa wale waliofanyiwa upasuaji siku za mwanzo.
Wanaendelea vizuri, wamesharuhusiwa kutoka katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) wako wodini wanaendelea na matibabu,” anasema Dk. Angela.
“Tunawashukuru wenzetu wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kwa kujitoa kwao kwani licha ya kutoa huduma za matibabu pia wametupatia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 ambavyo vinatumika katika kufanya upasuaji huu wa moyo unaoendelea,” amesema Dk. Angela.
Bingwa wa Moyo na Mishipa ya Damu kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu, Dk. Mohammad Shihata, anasema kambi hiyo imekuwa ikidhaminiwa na Mfalme Salman wa nchini Saudi Arabia kuwawezesha watoto kupata matibabu na kubadilishana ujuzi na madaktari wa JKCI.
Amesema timu nzima ya watu 26 kutoka nchini Saudi Arabia ambao ni waatalamu wa usingizi, waendesha mashine za moyo, wauguzi na madaktari wameshiriki katika kambi hiyo, ili kuhakikisha watoto wengi wanafanyiwa upasuaji wa moyo.
“Hii ni siku yetu ya tano na ni mara ya yangu ya saba kuja hapa nchini kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, siku zote tumekuwa tukipokea ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari wa JKCI katika kufanikisha utoaji wa huduma hii,” anasema Dk. Shihata.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED