MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, inatarajia kusikiliza mashahidi 40 na kupokea vielelezo 480 katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili wakazi wanne wa Dar es Salaam, wanaodaiwa kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh milioni 971.7.
Washitakiwa hao Frank Kagale, fundi wa mashine za kielektroniki za EFD, Awadhi Mhavile (39) Ally Msesya maarufu kama Ally Yanga (37) Mkazi wa Pugu na Salma Ndauka (38) Mkazi wa Sinza na Msimamizi wa Gereji ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 574
Wakili wa Serikali Tumpale Lawrence akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Medalakini na Wakili wa Serikali, Auni Chilamula alidai jana mbele ya Hakimu Kupa kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali.
Akisoma hoja hizo, Wakili Tumpale alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi Is-haq Kuppa kuwa mnamo mwezi Machi, 2023, TRA ilipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna risiti za kielektroniki zilizotolewa kutoka kwenye mashine zilizopotea au kuibwa kutoka kwa wamiliki halali na zinasambazwa isivyo halali.
Alidai kuwa kutokana na taarifa hiyo uchunguzi ulianza kwa kushirikiana na maafisa wa Jeshi la Polisi.
Alidai mnamo Julai 7, 2023 mtu aitwae Meshack Athanas dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda alikutwa na risiti za kielektroniki saba zenye kiasi cha Sh 128,500,000.
Alidai kati ya risiti hizo nne hizo zilikuwa zimetolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki mali ya Africa Harmony and Trade Ltd yenye namba 03TZ843040152 aliyesajiliwa kwa namba ya mlipakodi 159265420.
"Risiti mbili zilitolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki mali ya Tabisco Entreprises ltd yenye namba 03TZ442007272 na namba ya mlipa kodi ni 100219557 na risiti moja iliyotolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki mali ya Eco Consumer Products ltd yenye namba 03TZ442021550. Katika maelezo ya Athanas alieleza kupewa risiti hizo na Ally Omary Msesya ambae ni mtuhumiwa namba tatu," alidai Tumpale.
Katika tarehe hiyo hiyo, Athanas aliwaongoza wapelelezi katika ukamataji wa mshitakiwa Msesya na Julai 8, 2023 Athanas aliwaongoza wapelelezi kumkamata mshitakiwa Mhavile.
Alidai baada ya kukamatwa mshitakiwa namba Mhavile alikutwa na risiti za kieletroniki 11 zisizosahihi au za uongo zenye jumla ya Sh 133, 000,000 zikiwa zimetolewa kutoka kwenye mashine ya kieletroniki yenye namba 03TZ843040152 mali ya Africa Harmony Industry and Trade Ltd na mashine nyingine za kieletroniki 13 kampuni ya INCOTEXT zikisadikika kuwa za wizi au zimepatikana kinyume cha sheria na mashine hizo zilihodhiwa.
Pia alidai katika kumhoji mshitakiwa Mhavile alimtaja mshitakiwa namba moja Kagale kuwa ndiye mwenye mashine iliyotumika kutoa risiti hizo zisizo sahihi alizokutwa nazo.
"Kutokana na maelezo ya Mhavile juhudi za kumtafuta Kagale zilianza mara moja na Julai 19, 2023 wapelelezi walipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa Kagale ana rafiki wa kike aitwae Salma Ndauka ambae ni mshitakiwa namba nne," aliendelea kudai.
Julai 19, 2023 alikamatwa na katika upekuzi alikutwa na mashine 10 za kieletroniki aina ya INCOTEX ambapo mashine nane ndizo zilitambulika namba zake na mashine mbili hazikutambulika kwani zilifutika na kwamba mashine hizo zilihodhiwa.
Vilevile alidai, wakati wa kumhoji mshitakiwa Ndauka alimtaja pia Kagale kuwa ndiye mwenye mashine hizo.
Wakili Tumpale alidai kuwa Januari 16, mwaka huu Kalage alikamatwa na katika mahojiano alikiri kuwa mashine za kieletroniki alizokutwa nazo mshitakiwa Ndauka ni za kwake na alikiri kutumia mashine hizo kutoa risiti mbalimbali za kieletroniki zisizosahihi.
Kwa mujibu wa Tumpale, uchunguzi ulibaini kuwa mashine yenye yenye namba 03TZ443024331 mali ya Kampuni ya Oceanic Cachet katika kipindi cha kati ya Aprili, 2023 na Julai, 2023 ilitumika kutoa risiti ya za uongo au zisizo sahihi za Sh 1,932,096,214.28 na kutokana na kiasi hicho jumla ya kiasi cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh 294,726,540.37 hakikuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Alidai mashine yenye namba 03TZ442007272 mali ya Tabisco Enterprises ltd katika kipindi cha kati ya Aprili, 2023 na Juni, 2023 ilitumika kutoa risiti ya za uongo au zisizo sahihi za Sh 2,375,310,754.61 na kwamba kiasi cha Sh 373,537,333.9 kama VAT hakikuwasilishwa TRA.
Pia alidai mashine yenye namba 03TZ843040152 mali ya Africa Harmony lndusry and Trade ltd katika kipindi cha kati ya Mei, 2023 na Juni, 2023 ilitumika kutoa risiti ya za uongo au zisizo sahihi zenye jumla ya Sh 1,929240,063.00 na Sh 303,713,897.37 kama VAT hakikuwasilishwa TRA.
Alidai kutokana na hali hiyo, waliisababishia hasara ya Sh 971,977,772.32 na kwamba walipotosha mfumo na Kamishna Mkuu wa kwa kuonesha kuwa Kampuni ya Oceanic Cachet imefanya mauzo ya Sh 1,932,096,214.28, Kampuni ya Tabisco Enterprises ltd imefanya mauzo ya Sh 2,375,310,754.61 na Kampuni ya Africa Harmony lndusry and Trade ltd imefanya mauzo ya Sh 1,929240,063.00.
Wakili Tumpale alidai wakati wa uchunguzi ilibainika zaidi kuwa watuhumiwa wote wanne walikuwa wakiongoza na kuratibu genge la uhalifu wa makosa mbalimbali ambayo ni kutoa risiti zisizo sahihi, kutumia mashine za kieletroniki kwa namna ya kuupotosha mfumo au Kamishna Mkuu wa TRA, kukwepa kodi kinyume na sheria, kuisababishia hasara TRA na kutakatisha fedha.
Alidai kuwa washitakiwa wote walifikishwa mahakama hiyo kujibu mashitaka yanayowakabili.
Baada ya kusomewa hoja za awali, washitakiwa wote walikiri majina yao, maeneo wanayoishi na kufikishwa mahakamani hata hivyo, walikana mashitaka yote.
Washitakiwa Mhavile alikana dini iliyoandikwa kwamba ni mkristu akidai yeye ni muislamu, pia alikana kuwa fundi wa mashine za kielektroniki na kueleza kuwa yeye ni msambazaji wa mashine hizo.
Hakimu Kuppa aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 24, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa na washitakiwa wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED