RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa ahadi tano kwa wanafunzi 1,230,780 wanaofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi unaomalizika leo nchini, huku akisema ni zawadi kwao ambayo serikali inahakikisha inatimia.
Katika taarifa aliyoiandika kwenye WhatsApp Channel, Rais Samia alisema anawatakia kila la heri wanafunzi wa darasa la saba watakaomaliza elimu ya msingi leo.
“Mnatoka katika hatua moja ya elimu na malezi kwenda nyingine katika safari yenu ya kujiandaa kutoa mchango wenu wa maendeleo kwa taifa letu. Serikali imeandaa mazingira sahihi ili kufikia lengo,”alisema.
Alisema ahadi yake kwa wanafunzi hao katika safari ya elimu na maisha ambayo tayari inatekelezwa uhakika wa kupata nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza 2025 kwa kila atakayefaulu.
Nyingine ni miaka minne ya sekondari ya awali bila ada; miaka miwili ya kidato cha tano na sita bila ada; chuo cha ufundi katika kila wilaya kwa watakaochagua njia hiyo; na mikopo ya elimu ya juu kwa watakaofaulu kwenda vyuo vikuu.
Alisema ahadi hiyo inakwenda sambamba na kuendelea kuboresha sera za uchumi, ili kuzalisha fursa zaidi kwa kila mmoja kadiri wanavyoendelea kukua na kuingia katika nguvu kazi.
Kupitia Waraka wa Elimu Namba Tatu wa mwaka 2016, serikali ilitoa elimu ya awali hadi kidato cha nne bila malipo huku kupitia Waraka wa Elimu Namba Tano wa mwaka 2022, iliondoa ada kwa kidato cha tano na sita katika mfumo wa umma.
Kuondolewa kwa malipo hayo na kutolewa mikopo ya elimu ya juu ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mfunzo ya mwaka 2014 yenye lengo la kuhakikisha kuwa watoto wote wenye rika lengwa wanapata elimu bila kikwazo.
Aidha, ujenzi wa vyuo vya ufundi ni utekelezaji wa sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ya kuwapatia vijana elimu bora na ujuzi stahiki, ili kuinua kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi na kukidhi mahitaji ya soko.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2023/24, Waziri Prof. Adolf Mkenda alisema serikali itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu 223,201 hadi 252,245.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Said Ally Mohamed, kati ya watahiniwa waliosajiliwa wavulana ni 564,176 sawa na asilimia 45.84 na wasichana ni 666.604 sawa na asilimia 54.16.
Alisema watahiniwa 1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani kwa Lugha ya Kiswahili na 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya kwa lugha ya Kiingereza, lugha walioitumia wakati wa kujifunza.
Alisema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosajiliwa ni 4,583, kati yao 98 ni wasioona, 1,402 wenye uoni hafifu, 1,067 wenye uziwi, 486 ni wenye ulemavu wa akili na 1,530 ni wenye ulemavu wa viungo.
Pia alisema mitihani hiyo itajumuisha masomo sita ambayo ni Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi na Uraia na Maarifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED