Madalali wamkaba mwandishi kwenye bomoabomoa Dar

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:35 AM Sep 12 2024
Mabaunsa wa Kampuni ya Bilo Star Debt Collection Co. Ltd, wakiwatoa nje wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba kitalu namba 266, Barabara ya Ally Khan, eneo la Upanga Magharibi, jijini Dar es Salaam jana inayosemekana kuwa na mgogoro.
PICHA: IMANI NATHANIEL
Mabaunsa wa Kampuni ya Bilo Star Debt Collection Co. Ltd, wakiwatoa nje wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba kitalu namba 266, Barabara ya Ally Khan, eneo la Upanga Magharibi, jijini Dar es Salaam jana inayosemekana kuwa na mgogoro.

MPIGAPICHA wa Gazeti la Nipashe, Imani Nathaniel, jana alishambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni madalali wa mahakama waliokwenda kuvunja nyumba eneo la Upanga Magharibi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana akiwa Kituo cha Polisi Selander Bridge kwa ajili ya kutoa maelezo yake, Mwandishi Imani alisema: “Ilikuwa ni majira ya saa nane mchana alipoelekea katika eneo hilo ambapo kulikuwapo na zoezi la kuhamisha watu waliokuwa wamepanga katika nyumba namba 266 barabara ya Alykhan Upanga.”

Alisema alifika eneo hilo ili kuanza kutekeleza wajibu wake kama mwandishi kwa kuanza kupiga picha wakati wa kuondoa vitu vya wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo.

Alisema wakati anaanza kupiga picha, ghafla alishambuliwa kwa vipigo na mabaunsa waliokuwa wameambatana na madalali wa Kampuni yaKampuni ya Bilo Star Co. Ltd.

“Walinipiga na kuninyang’anya kifaa changu cha kazi (kamera) pamoja na kunifunga pingu katika mikono yangu. Walifuta  picha zote nilizokuwa nimepiga kupitia kamera yangu.

“Baada ya muda nilifanikiwa kumwona kiongozi wao nilimweleza hali hiyo, kisha aliamuru nirejeshewe kamera, na kuachiwe huru na kunitaka niondoke katika eneo hilo mara moja. 

Mwandishi aliona barua ya notisi ya kuhama eneo hilo yenye kumbukumbu  Na:BSDC/DCR/09/2024/04 yenye kichwa cha barua “Notisi ya siku saba kuhama kwenye nyumba/eneo plot No, 266 iliyoko Upanga, Dar es Salaam iliyotolewa na Julitha Bartalomeo kwa niaba ya kampuni.

Barua hiyo ilionyesha kutolewa na kampuni hiyo kuwataka wapangaji katika nyumba hiyo kuondoka ndani ya siku saba kwa amri ya mteja wao aliyetambulishwa kwa majina ya Jammale Mohamed Said.

Katika barua hiyo pia ilionekana nakala kuwasilishwa kwa mkuu wa kituo cha polisi pamoja na ofisi ya serikali ya mtaa (haijataja kituo kipi cha polisi wala ofisi ya serikali ya mtaa).

Kutokana na tukio hilo, Nathanael alisema ameripoti Kituo cha Polisi Selander saa 9:33 alasiri kwa lengo la kutoa taarifa kutokana na shambulio hilo alilofanyiwa.