DC aagiza kukamatwa wanafunzi wanaozurura

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 12:35 PM Mar 28 2024
Njombe yaamua kupambana na utoro mashuleni.
PICHA: Thapelo Morebudi
Njombe yaamua kupambana na utoro mashuleni.

MKUU wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa amewaagiza watendaji wa kata, mitaa na vijiji wilayani hapa kuwakamata wanafunzi ambao wanazurura mitaani wakati wa masomo, ili kukabiliana na tatizo la utoro pamoja na ukatili wa kijinsia.

Agizo hilo amelitoa wakati wa kikao cha wadau wa elimu cha Halmashauri ya Mji Njombe kilichoenda sambamba na utoaji tuzo kwa shule zilizofanya vizuri kitaaluma kilichofanyika mkoani hapa.

“Mtoto atakayeonekana anazagaa wakati wa masomo achukuliwe, atafutwe mzazi wake na mzazi wake awajibishwe na jamii husika kwa sababu haiwezekani watoto tukawapoteza, watoto kwenye utoro wanafanyiwa vitu vibaya sana kuna mambo mengi yanatokea huko mtaani lazima tuwalinde watoto wetu,’’ amesema Kasongwa.

Hata hivo amesema kuwa kila kata na mitaa zinapaswa kutengeneza mkakati wa kuwalinda watoto na kutaka jambo hilo kufanyika kwa haraka kwa sababu ya kuonekana kuna wimbi kubwa la watoto mitaani.

“Mimi mwenyewe nitamchukulia hatua Mtendaji wa Kata wa eneo hilo kwa maana ya kusema hivyo ningeomba sana watendaji wa kata, mitaa na vijiji washirikiane na walimu wakuu la sivyo itakuwa jambo ambalo si shirikishi,” amesema Kasongwa.

Kwa upande wake, Mkurugezni wa Halmashuari ya Mji Njombe, Kuruthum Sadick amewataka walimu kuzingatia uweredi na kuacha kufanya vitendo vizivyofaa kwa wanafunzi.

“Walimu badala ya kuwa ni wazazi tunajisaau tunakengeuka, tumekuwa na kesi nyingi za walimu kufanya ambavyo sivyo kwa watoto kwa hiyo niwaombe walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kwamba ambaye mnamuona anatabia ambayo ni mbaya mchukulieni hatua,” amesema Sadick.

Awali Ofisa Elimu Taaluma Msingi Halmashauri ya Mji Njombe, Bryson Kingililwe amesema zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na hivyo kushindwa kufikia malengo yalizokusidiwa.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu mkubwa wa miundombinu ya madarasa, matundu ya vyoo, utawala, maktaba na nyumba za walimu.

“Kwa upande wa uhaba wa nyumba za walimu hasa ukizingatia shule nyingi zimejengwa maeneo yasiyo na makazi ya watu ambako nyumba za kupanga hazipo hata zikipatikana hazina ubora hii hufanya walimu kutokuwa na mazingira ya kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema Kingililwe.

Baadhi ya wakuu wa shule za serikali akiwemo Mkuu wa Shule ya Sekondari Yakobi, Deogratias Msagati amesema moja ya sababu iliyosababisha shule yake kufanya vizuri kitaaluma ni pamoja na kukutana na wazazi na kuwaeleza kuhusu umuhimu wa kushiriki malezi kwa watoto.