Chuo chahamasisha utalii wa ndani

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:27 PM Apr 12 2024
Watumishi katika Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto pamoja na Manispaa ya Shinyanga wakiangalia Kivutio cha Chemchem ya Maji ya Moto Uzogore ambayo ukiyaoga au kunawa unaondoa Mikosi yote.
PICHA: MARCO MADUHU
Watumishi katika Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto pamoja na Manispaa ya Shinyanga wakiangalia Kivutio cha Chemchem ya Maji ya Moto Uzogore ambayo ukiyaoga au kunawa unaondoa Mikosi yote.

KATIKA kuhamasisha utalii wa ndani, Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto na Manispaa ya Shinyanga, wametembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika Manispaa hiyo, sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha utalii nchini.

Ziara hiyo imefanyika jana kwa kutembelea baadhi ya vivutio, ambapo manispaa hiyo ina vivutio 13 vilivyopitishwa na Bodi ya Utalii Tanzania.

Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Paschal Shiluka akizunguma kwenye ziara hiyo, amesema wao kama taasisi inayojishughulisha na masuala ya afya, wamekuwa wakimuunga mkono Rais Samia katika sekta mbalimbali, na kwamba ndani ya miaka minne mfululizo, wameshatembelea karibu hifadhi zote za taifa, sambamba na kupanda Mlima Kilimanjaro.

“Sisi kama chuo, tuna mkubali sana Rais Samia kwa utendaji wake kazi, ndiyo maana tuna muunga mkono. Katika sekta ya utalii, hakuna mbuga ambayo hatujafika na tumekwenda kutalii hadi Zanzibar, yote hii ni kuunga juhudi za Rais Samia kuhamasisha utalii,” amesema Shiluka.

Naye Mkuu wa Idara ya Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga, amesema katika manispaa hiyo kuna jumla ya Vivutio vya utalii 13, lakini katika ziara hiyo wametembelea vinne, huku akitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga watembelee vivutio hivyo, ili kuunga juhudi za Rais Samia kuhamasisha Utalii.

Amesema sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa, na kumpongeza Rais Samia kwa kuhamasisha Utalii hapa nchini.

Aidha, katika ziara hiyo vivutio vya utalii ambavyo vimetembelewa ni pamoja na chemchem ambayo inatoa maji ya moto iliyopo Uzogore, ambapo wenyeji wanaamini ukiyatumia maji yake, unaondoa mikosi mbalimbali, na inadaiwa kuna ushuhuda mwanamke ambaye alikuwa tasa, alipotumia maji hayo alipata mtoto.

Vivutio vingine vilivyo tembelewa ni eneo la Makumbusho Mazingira Center, eneo jingine ni Mahali ambapo Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipowahutubia Watanzania wakati wa kudai Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Eneo jingine ni Mahali ambapo Bendera ya Mkoloni Mwingereza ilipotelemshwa na kupandishwa Bendera ya Tanganyika mara baada ya kupata Uhuru, pamoja na kutembelea pia makaburi nane ya wapiganaji wa Jeshi la Kiloloni yaliyopo Mlima wa Old Shinyanga.