Bodi ya Wakurugenzi CRB yafurahishwa utekelezaji mradi uwanja wa ndege, ujenzi SGR Shinyanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:47 PM Oct 03 2024
Bodi ya Wakurugenzi CRB yafurahishwa utekelezaji mradi uwanja wa ndege, ujenzi SGR Shinyanga
Picha: Mpigapicha Wetu
Bodi ya Wakurugenzi CRB yafurahishwa utekelezaji mradi uwanja wa ndege, ujenzi SGR Shinyanga

Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya CRB wamekagua na kuridhishwa na ujenzi wa Mradi wa Ukarabati na Uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga pamoja na Mradi wa kusanifu na kujenga njia ya reli ya kisasa na stesheni ya Standard Gauge (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka, iliyoko eneo la Malampaka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRB Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameeleza hayo wakati akikagua Ujenzi wa Mradi wa Ukarabati na Uboreshaji wa Uwanja wa Ndege unaotekelezwa na Mkandarasi China Henan International Cooperation Group (CHICO) pamoja na Mradi wa SGR wa kusanifu na kujenga njia ya reli ya kisasa ya Standard Gauge unaotekelezwa kwa ubia na Makandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Corporation (CRCC) mkoani Shinyanga.

“Tumeona na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi CHICO kwa kuzingatia ubora wa kazi kwa kufuata sheria za Usajili wa Makandarasi, matumaini yetu kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati ili uanze kuleta manufaa ya kijamii na ya kiuchumi”, amesema Mhandisi Nyamhanga. 

Pamoja na hayo amempongeza Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), na China Railway Construction Corporation (CRCC) kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kusanifu na kujenga  stesheni na njia ya reli ya kisasa (SGR), kipande cha Isaka - Mwanza chenye urefu wa kilometa 341.

“Tunaona kwamba mradi huu unaendelea vizuri na utakapokamilika mpaka Mwanza utaleta manufaa makubwa sana kwa nchi yetu kama tulivyoanza kuona kwa kipande kilichokamilika kutoka Dar es salaam, Morogoro hadi Dodoma”, amesema Mhandisi Nyamhanga.

Hata hivyo Mhandisi. Nyamhanga amepongeza hatua iliyofanywa na Makandarasi wa miradi hiyo kwa ushirikishwaji mzuri kwa makandarasi wa ndani katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutekeleza miradi mikubwa nchini. 

“Moja ya majukumu ya Bodi ni kuwaendeleza Makandarasi wa ndani kwa kuhakikisha wanashirikishwa katika miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya nchini ili kuwajengea uwezo” alisema Mhandisi Nyamhanga.

Aidha ametoa wito kwa Makandarasi wote nchini kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na thamani wa mikataba ya miradi ya ujenzi.

Naye Naseer, Mhandisi Mkazi Mshauri wa mradi kutoka SMEC Engineering International, amesema kuwa hadi sasa wameshakamilisha ujenzi wa ukarabati na uboreshaji wa  uwanja wa ndege wa shinyanga kwa asilimia 72 ikiwa ni pamoja na njia ya kurukia ndege yenye urefu wa 2.2km.

“Mpaka sasa tumeshakamilisha vipengele muhimu, ikiwa ni pamoja na njia ya kurukia ndege, jengo la abiria, wigo na mfumo ya kuongoza ndege”, amesema Mhandisi Naseer.

Pamoja na hayo Mkandarasi CHICO anayetekeleza mradi huo ameahidi  kukamilisha ujenzi kwa wakati kwa kuzingatia mkataba.

Sambamba na hayo, Mhandisi Samweli Mwambungu, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa mradi wa Ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga unahusisha ujenzi wa kiwanja cha ndege na jengo la abiria. 

“Hadi kufikia sasa Mkandarasi amefanikisha ujenzi wa barabara ya kurukia ndege na kazi kubwa imebakia katika umaliziaji wa jengo la abiria na kufikia mwezi Novemba watahakikisha ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 100 ili uanze kutoa huduma kwa wananchi”, amesema Mhandisi Mwambungu.

Kwa upande wake Justine Mazinge, Mhandisi wa Viwango na Ubora katika Mradi wa Ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka amesema maendeleo ya mradi hadi sasa  ni asilimia 60.5 ambapo ujenzi mkubwa wa matuta na miundombinu ya madaraja umekalimia huku ujenzi wa reli na miundombinu ya umeme ikiendelea kufanyika.

Aidha Mkandarasi CCECC anayetekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isiaka ameahidi kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia ubora wa kazi kwa mujibu wa mkataba.