Wabunge Kenya waomba ulinzi kujadili hoja kumng’oa Gachagua

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:54 PM Oct 03 2024
Makamu wa Rais nchini humo Rigathi Gachagua.
Picha:Mtandao
Makamu wa Rais nchini humo Rigathi Gachagua.

BAADHI ya wabunge nchini Kenya wana wasiwasi kuhusu usalama wao katika kipindi cha kuanza kujadili hoja ya kumtimua Makamu wa Rais Rigathi Gachagua, baada ya kuwasilishwa hoja ya kutokuwa na imani naye.

Aidha, imeelezwa kuwa wabunge hao walimsihi Spika wa Bunge, Moses Wetang'ulah kuingilia kati kwa kuagiza mamlaka husika kuimarisha usalama wao na wa Rais William Ruto wakati wa shughuli hiyo.

Mbunge wa Kikuyu na kiongozi wa walio wengi Kimani Ichung'wah amedai kuwa wabunge walindwe ipasavyo sio tu katika maeneo ya bunge bali hata majumbani mwao. 

Pia wabunge hao walielezea wasiwasi wao kuhusu usalama wao baada ya kupewa notisi ya hoja ya kumshtaki Makamu wa Rais nchini humo Rigathi Gachagua.

Imebainishwa kuwa jumla ya wabunge 291 walitia saini kuunga mkono hoja hiyo. Na kwamba Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, alipothamini ukubwa wa suala hilo mbele ya Bunge, alielezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa wabunge wanaoshiriki katika kesi dhidi ya Gachagua.

Amedokeza kwamba wale wanaounga mkono hoja hiyo wanaweza kutishwa au kuwekwa njiani au hata kukabiliwa na hali mbaya ya kiusalama katika jitihada za watu wasiojulikana ili kukandamiza kesi hiyo.

Mbunge huyo amerejelea matukio ya Capitol Hill mnamo 2021 wakati wafuasi wa rais wa zamani wa Merika Donald Trump walipovamia Bunge la Congress, na kuwafanya wabunge waliojawa na hofu kujificha.

“Nataka kupata uhakika wako kwamba wabunge 291 waliotia saini hoja hii ya mashtaka, ulinzi na usalama wao utakuwa wa uhakika, tunataka wote wajitokeze hapa siku ya kupiga kura, mnalijua hili jambo na mnalijua nini kinaweza kutokea hapa," Junet alisema.

Mbunge wa Daadab, Farah Maalim ameshiriki katika wasiwasi huo huo, akiomba usalama zaidi sio tu kwa wabunge hao bali pia kwa Rais William Ruto.

"Mimi pia naungana na wenzangu katika hili. Lakini nataka tu kuzungumzia suala muhimu zaidi, sio tu kulinda maisha ya wabunge 291 ambao wametia saini huko. Ni lazima tulinde mfumo. IG lazima alinde maisha yetu.

“Rais mzembe, jambazi yeyote mzembe anaweza kuamua kubadili historia...kama Mungu angezuia jambo lolote lisitokee kwa rais wetu, basi tunalo jambo kubwa zaidi la kuhangaikia rais wetu hadi hoja hii iishe,” alisema Maalim.

KUHUSU RUTO

Wakati sakata hilo likiendelea ilielezwa kuwa Rais Ruto aliendelea kujitenga kabisa na matatizo yanayomkabili Naibu wake Gachagua, ambaye kazi yake sasa imo hatarini.

Imeelezwa kuwa ukimya mkubwa wa Rais Ruto kuhusu mchakato unaomkabili naibu wake umesababisha wengi kufikia hitimisho kwamba anaunga mkono hoja hiyo.

Imeelezwa kuwa Rais Ruto alikuwa ndani ya eneo la Ikulu wakati ilani ya kumwondoa Gachagua ikiwasilishwa rasmi katika Bunge la Kitaifa Oktoba 1, mwaka huu.

Imeelezwa kuwa Waziri wa Kazi na Ulinzi wa Jamii Alfred Mutua, ambaye ni wa chini ya Rais Ruto kwenye Baraza la Mawaziri, pia aliunga mkono hoja hiyo ya kumwondoa Gachagua.

Wakati wa kuwasilisha ilani ya hoja hiyo Jumanne, Mbunge wa Kibwezi Mwengi Mutuse, aliyekuwa mwendeshaji wa hoja hiyo, ameweka madai kadhaa juu ya jina la Gachagua, akiahidi kutoa ushahidi wa kila moja katika jitihada zake za kuwashawishi wenzake kumwondoa naibu wa rais.

KTN