Majaliwa: Theluthi moja ya watoto nchini wana udumavu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:40 PM Oct 03 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema licha ya juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi nchini na kimataifa bado kuna tatizo kubwa la udumavu ambako theruthi moja ya watoto nchini wana udumavu.

Majaliwa alitoa kauli hiyo leo Alhamisi mkoani Mwanza wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 10 wa Wadau wa Lishe nchini.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) mwaka 2018 inaonesha kuwa theruthi ya watoto nchini wamedumaa.

Amesema licha ya tatizo hilo bado kuna ongezeko la magonjwa sugu yasiyoambukiza yanayotokana na lishe duni hivyo kuwataka wadau kuongeza nguvu katika utekeleza wa malengo ya afua ya lishe.

Aidha, amesema kutokana na tatizo hilo upo umuhimu wa wadau mbalimbali kuandaa mjadala mpana wa kitaifa, ili kuleta msisitizo katika utekelezaji wa mipango ambayo tayari imewekwa na serikali pamoja na wadau mbalimbali.

Kadhalika ameagiza kutolewa kwa elimu na msisitizo kuhusu lishe katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuifanya kuwa ajenda ya kitaifa katika nyumba za ibada pamoja na kwenye vyombo vya habari.

“Juhudi za serikali zinaendelea zikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kusainisha mikataba wakuu wote wa mikoa kuhakikisha wanatekeleza afua hiyo niagize TAMISEMI kuhakikisha inasimamia kwa ukamilifu mikataba hiyo itekelezwe,”alisema Majaliwa.

Aidha, aliwataka wadau wa maendeleo likiwemo shirika la GAIN Tanzania pamoja na SANKU kuimarisha utekelezaji wa programu ya uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula hususani katika maeneo ya vijijini.

 “Lengo ni kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa uwepo wa mashine za bei nafuu za kuchanganyia virutubishi na upatikanaji wa virutubishi vinavyozalishwa kwa kutumia malighafi inayopatikana ndani ya nchi kwa bei nafuu,”amesema Majaliwa.

 Awali akitoa tathimini ya Mkutano huo Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Dk.Jim Yonazi amesema zaidi ya watoto milioni tatu nchini wana tatizo la udumavu hali aliyoitaja kuwa mbaya zaidi kwa Taifa la baadaye.

Kadhalika alisema zaidi ya watoto 600,000 wana utapiamlo mkali na wakadili sambamba na ukondefu wa asilimia 3.5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015.

Meneja wa Mradi, Programu ya Uimarishaji Chakula kutoka Shirika la GAIN Tanzania Archard Ngemela, amesema ili kukabiliana udumavu nchini kuna uhitaji mkubwa wa jamii kupata unga uliorutubishwa.

Amesema katika kuisaidia jamii kupata unga wenye virutubisho shirika hilo limekuja na mradi wa mashine yenye uwezo kusindika unga kwa kuchanganya virutubisho muhimu ikiwa na lengo pia la kuzisaidia shule kupata huduma hiyo muhimu.

“Wazazi wamekuwa wakichanga mahindi shuleni kwaajili ya chakula cha watoto, lakini wamekuwa hawapati unga uliorubtubishwa hivyo kufanya hali ya udumavu kwa watoto kuendelea kuwa kubwa nchini,”amesema Ngemela.

Naye Meneja Mradi wa Afya na Lishe kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kutoka shirika la World Vision Tanzania Shukrani Dickson, amesema bado jamii imeshika mila na desturi potofu zinazodidimiza mwanamke na kumfanya mwanaume kuwa na uamuzi wa kipi kitaliwa nyumbani na kwanini.

Shukrani amesema kukabiliana na hali hiyo iliyobainika katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga, shirika hilo limeanza kumshirikisha kwa karibu mwanaume katika afua za lishe, ili kuondoa ule utamaduni wa kuuza mazao na vitu muhimu vyenye lishe kisha kuiacha familia na chakula cha aina moja.

“Kupitia modo yetu ya ‘men care’ tunahakikisha tunatoa elimu kwa jamii hasa kwa wanaume kujua umuhimu wa vyakula vy asili kama vile mayai, kuku, choroko na vingine ambavyo mara nyingi wamekuwa wakiviuza na kuiachia familia mahindi pekee,”amesema Shukrani.