Askofu azikwa kikanisa, ripoti polisi yasubiriwa

By Paul Mabeja ,, Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 09:25 AM May 21 2024
Waombolezaji wakiuaga mwili wa marehemu Askofu Bundala.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waombolezaji wakiuaga mwili wa marehemu Askofu Bundala.

KUKIWA na maswali mengi juu ya kifo cha Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist Tanzania (MCT), Joseph Bundala (55), anayedaiwa kujinyonga, hatimaye mwili wake ulizikwa jana kwenye viwanja vya kanisa hilo Ihumwa, jijini Dodoma.

Wakati wa maziko ya mwili huo jana, uongozi wa kanisa hilo haukuweka bayana kilichosababisha uamuti kwa kiongozi wake huyo, ukisisitiza unasubiri ripoti za uchunguzi.

Askofu Bundala alikutwa amefariki dunia, akidaiwa kujinyonga ndani ya ofisi yake iliyoko kanisani huko, Mtaa wa Meriwa, Kata ya Ipagala, jijini hapo Mei 16, mwaka huu.

Akiongoza ibada ya kuuga mwili wa Askofu Bundala iliyofanyika nyumbani kwake Ihumwa, jijini Dodoma, Makamu  Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Samweli Nyanza, alisema yote yaliyotokea na yanayosemwa wanamwachia Mungu.

"Wanasema sana kuhusu kanisa lakini kanisa litazidi kusimama imara, taarifa nyingi za vyombo vya habari zimeongezwa chumvi, maneno haya hata kwenye kanga yapo, sisi hatutaogopa maneno," alisema askofu huyo.

Alieleza kuwa baada ya tukio hilo kumekuwa na taarifa nyingi ambazo wanazipa tafsiri zina lengo la kudhoofisha kanisa. 

Alisema kuwa wamefarijiwa na waraka wa Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajab, aliyewataka kungalia mambo mawili; heshima ya kiongozi na heshima ya kanisa.

Askofu Nyanza alisema kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa yenye misingi mizuri, akieleza kuwa Askofu Bundala alikuwa mcheshi na atakumbukwa katika maisha yake.

Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa shule binafsi Mkoa wa Dodoma, Mbunge wa zamani wa Dodoma, David Malole alisema umoja huo umepoteza mwanachama aliyekuwa na ushirikiano mzuri.

Diwani wa Ipagala, Dotto Gombo alisema watamkumbuka Askofu Bundala kutokana na kuwa mpenda maendeleo na aliyekuwa na ushirikiano mzuri na jamii.

Askofu Mkuu wa Elimu Pentekoste, Peter Konki, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa hiyo kwa kuwa Askofu Bundala alikuwa na ushirikiano mkubwa.

Akisoma wasifu wa marehemu, mwanafamilia Kikoti Lissu alisema Askofu Bundala alizaliwa Machi 18, 1969 kijiji Bubinza, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga akiwa mtoto wa sita kati ya 11 kwa Michae Bundala na mkewe Scolastika Pius.

Baada ya masomo ya sekondari alijiunga na jeshi na baadaye akajiunga na kanisa kutoa huduma za kiroho, akianzia uinjilisti, uchungaji na hatimaye askofu.

Alisema kuwa Askofu Bundala ameacha mke na watoto watatu, akisisitiza chanzo cha kifo chake kinachunguzwa.

Mwili wa Askofu Bundala uligundulika Meio 16 saa moja usiku ukiwa unaning’inia ofisini kwake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, alisema jeshi hilo linachunguza tukio hilo. Mwili uligundulika ndani ya ofisi yake iliyoko katika kanisa hilo. 

Alisema kuwa uchunguzi katika eneo la tukio ulibaini kuwapo ujumbe unaoeleza kinachodaiwa sababu za kujinyonga ni madeni na mgogoro uliopo katika uendeshaji shule binafsi. Hata hivyo, kiwango cha fedha anachodaiwa hakijatajwa katika ujumbe huo.