Waziri aitwisha zigo ALAT maslahi ya umma

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:03 AM Apr 27 2024

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed.
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amezitaka Jumuiya za Tawala za Mikoa (ALAT) kujipambanua kwa kutetea maslahi ya umma ili kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii.

Waziri Masoud alisema hayo juzi wiki wakati akifunga Mkutano wa Mkuu 38 wa ALAT, uliofanyika visiwani hapa.

Alisema kama viongozi wa jumuiya hawatakuwa wakweli na kuendelea kuoneana  aibu, ni ndoto kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na wananchi.

"ALAT ni chombo muhimu ambacho kinatakiwa kusimamia uadilifu, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, kutetea maslahi hasa ya wanyonge," alisema Waziri Masoud.

Aliwataka wajumbe wa ALAT kujitahidi kujenga serikali za mitaa zenye uwajibikaji, uwazi na zenye kusikiliza sauti za wananchi kwa kusimamia rasilimali  zilizopo.

Waziri Masoud alisema changamoto nyingi zinazotokea  kwa wananchi, ALAT ndiyo wa kwanza wanaotakiwa kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kufika serikali kuu.

Pia Waziri Masoud aliishukuru ALAT kwa namna ilivyofanya jitihada kubwa katika kuanzishwa kwa Jumuiya ya Tawala za Mikoa Zanzibar (ZALGA).

Alisema ushirikiano baina ya ZALGA na ALAT ni muhimu  katika kuhakikisha  kwamba sauti za mamlaka za serikali za mitaa zinapaishwa katika kuwaletea maendeleo wananchi.

"Niwasihi ushirikiano huu uendelee  kudumishwa ili kuhakikisha tunafikia malengo ya sera hii"alisema Waziri huyo.

Mwenyekiti wa ALAT, Murshid Ngeze, alisema ni vyema mikutano ya ALAT ifanyike kabla ya vikao vya Bunge na Baraza la Wawakilishi ili hoja zitakazoibuliwa ziweze kujadiliwa katika vikao hivyo.

"Hii itasaidia kwa wajumbe waliopo katika vikao hivyo kutoa mawazo yao na kuchukuliwa ili kufanyiwa kazi katika kipindi cha bajeti bungeni".alisema.