Wastaafu 13,000 walipwa mafao kwa kikokotoo kilichoboreshwa

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 11:10 AM Dec 30 2024
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yessaya Mwakifulefule.
Picha:Mtandao
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yessaya Mwakifulefule.

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unaendelea kutekeleza agizo la serikali ulipaji mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa.

Uongozi wa mfumo huo umesema kuwa tayari Sh. bilioni 126 zimelipwa kwa wastaafu 13,167 kuanzia Julai Mosi hadi kufikia Desemba mwaka huu.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yessaya Mwakifulefule alisema hayo wakati wa mafunzo na utoaji elimu kuhusu mfuko huo kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro.

Mwakifulefule alisema mfuko ulianza kulipa mafao kwa wastaafu kuanzia Septemba mwaka huu kwa mujibu wa tamko la serikali lililotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Alisema utekelezaji wa utoaji malipo hayo umekuwa wa aina mbili; asilimia mbili ambayo inalipwa moja kwa moja na mfuko huo na kuna malipo ya asilimia saba ambayo yanalipwa na serikali (mwajiri).

Alisema katika malipo ya asilimia mbili, kuna wale waliostaafu kwa mujibu wa sheria kuanzia Julai Mosi 2024, hao wameingia katika sheria mpya ambayo imeboreshwa bungeni.

Mwakifulefule alisema kundi hilo walilipwa jumla ya wastaafu 983 hadi kufikia Desemba mwaka huu, lakini pia wale wa asilimia saba walilipwa wastaafu 1,984 ambapo katika kipengele hicho mfuko umewalipa wastaafu 2,967.

Alifafanua kuwa ukiacha hao, pia kuna wale ambao walikuwa wanalalamikia mapunjo ambao walilipwa kwa mujibu wa sheria ya kikokotoo kilichokuwapo mwaka 2022.

Meneja huyo alisema kuwa hao nao walishalipwa kwa viwango vinavyoridhisha kwa maana baada ya kuboreshwa kwa sheria ya kikokotoo kipya.

Alisema PSSSF ililazimia kurejea tangu walipostaafu na kuanza kuwalipa mapunjo yao na katika kundi hilo waliolipwa na mfuko ni 3,364 ambao ni asilimia mbili na malipo yao ambapo wale wa asilimia saba kutoka serikalini walikuwa ni 9,803.

Meneja huyo alisema kuwa katika kundi hilo palikuwa na jumla ya wastaafu 13,167 na katika eneo hilo, mfuko umelipa jumla ya Sh. bilioni 126 kwa wastaafu wa makundi hayo mawili.

Meneja wa PSSSF Kanda ya Mashariki, Zaida Mahava, alisema kutokana na maboresho makubwa ya huduma yaliyofanyika kwa ngazi ya kanda, malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa.

"Kwa sasa tumefikia sehemu nzuri kwa kuwa tumepunguza kero, tumepunguza malalamiko na hili ndilo lengo letu kuu kuhakikisha kwamba tunahudumia wanachama vizuri na kwa wakati," alisema Mahava.

Alisema kuwa katika uboreshaji utoaji wa huduma, PSSSF inaendelea kutoa elimu na mafunzo ya namna ya kutumia mfumo wa PSSSF Kidigitali kwa wanachama wake hususani walioko maeneo ya vijijini.

Mahava alisema mafunzo hayo ambayo ni endelevu, yataendelea kutolewa ili kuyafikia makundi yote bila kumwacha mtu yeyote nyuma kwenye falsafa ya PSSSF Kiganjani.

Awali, Mwenyekiti wa MoroPC, Nickson Mkilanya alipongeza PSSSF kwa kuandaa fursa ya mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa huo, akisema kuwa wako tayari kushirikiana katika kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhusu huduma zinazopatikana na kutolewa na mfuko huo nchini.