ZAIDI ya vikundi 60,000 vya ujasiriamali vilivyoundwa na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) vimekusanya Sh.bilioni 7.9 kwa ajili ya kukopeshana na kuepukana na mikopo umiza inayosababisha kuwarudisha nyuma kimaendeleo wanapoweka dhamana ya mali zao.
Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano kutoka Makao Makuu ya TASAF, Japhet Boaz, aliyabainisha haya katika kikao cha kujengwa uelewa viongozi na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini na kusema, vikundi hivyo mpaka sasa vinawanachama 800,038 nchini nzima.
Alisema wanufaika TASAF wameweza kuunda vikundi vya ujasiriamali 60,342 na kujiwekea akiba ya Sh.bilioni 7.9 nchini nzima na kukopeshana Sh.bilioni 3.2 katika mzunguko wao kupeana na kurejesha na imewasaidia kuondokana na mikopo umiza iliyokuwa inawarudisha nyuma kimaendeleo hasa wanapoweka dhamana ya nyumba zao.
Boaz alisema kaya 84,674 zimefikiwa na kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara na kusimamisha shughuli za kiuchumi zenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 31 na wataendelea kutoa elimu hiyo kila wanapowafikia, ili kuhakikisha walengwa wote wanaondokana na wimbi la umasikini uliokidhiri.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Annamringi Macha, alisema baadhi ya wananchi hawaelewi namna TASAF ilivyoweza kukuza uchumi wa kaya na kuondokana na umasikini uliokithiri na kuwataka kuendelea kutoa elimu, ili kila mmoja wao atambue adhima ya serikali katika kupambana na janga la umaskini kwa wananchi wake.
Macha alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuelimisha wananchi juu ya shughuli wanazozifanya walengwa na kupata ruzuku ili kuondoa tafsiri watu kuwa wanafanyishwa kazi kama wafungwa jambo ambalo sio kweli na ni sehemu moja wapo ya kujiingia kipato katika miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa.
Mmoja wa wanufaika hao, Rose Zakaria alisema waliamua kuanzisha mchezo wa hisa na kukopeshana ili kutojiingiza kwenye mikopo umiza ambayo inawafilisi na kuwarudisha nyuma kimaendeleo na wanakopeshana na kurejesha ndani ya siku 90 na kufanya hivyo ni sehemu ya kusaidiana wenyewe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED