Wananchi Mbeya hawataki risiti wanapofanya manunuzi

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 10:20 AM Apr 24 2024
Mashine ya EFD ikitoa risiti.
Picha: Mtandao
Mashine ya EFD ikitoa risiti.

WANANCHI mkoani Mbeya wanadaiwa kutokuwa na utamaduni wa kudai risiti wanaponunua bidhaa ama huduma mbalimbali, hali ambayo inasababisha migogoro baina ya wafanyabiashara na maofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Wafanyabiashara walitoa malalamiko hayo juzi wakati maofisa wa TRA walipofanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka na kwenye masoko kwa lengo la kuangalia namna wafanyabiashara wanavyotekeleza sheria za nchini.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Mandela Ndelwa alisema baadhi ya wananchi huwa wananunua bidhaa na kuondoka nazo bila kuchukua risiti, hata kama watakumbushwa na wafanyabiashara jambo ambalo alisema linahitaji elimu.

Alisema baadhi huwa wanapuuzia kwa kusema risiti hazina maana kwao zaidi ya bidhaa ambazo wanakuwa wamezinunua na hivyo wakishakabidhiwa bidhaa wanaondoka na kuacha risiti hata kama imeshatolewa.

“Kwa mfano hapa kuna dada amekuja amenunua chombo lakini nilipompatia risiti ameikataa kidai kuwa ni uchafuzi wa mazingira na hivyo akaondoka, sasa hili jambo linatugombanisha na serikali,” alisema Ndelwa.

Naye Erick Mwaitege alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wakikamatwa na maofisa wa TRA huwa wanarudi nao kwenye maduka na kuwaonyesha sehemu waliponunua bidhaa jambo ambalo linasababisha migogoro.

Alisema wakati mwingine maofisa wa TRA wakifika na wateja hao wanakuta risiti zilishatolewa na kwenye mfumo zinaonekana lakini wateja walizipuuzia na kuziacha.

Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Musibu Shaban alisema kwa mujibu wa sheria za nchi ni kosa kwa mfanyabiashara kuuza bidhaa bila kutoa risiti na kwamba akikamatwa kuna adhabu ambazo zinaweza kuwaumiza.

Alisema adhabu zinazotolewa kwa wafanyabiashara wasiotoa risiti ni faini isiyopungua Sh. milioni 1.5 ama mara tatu ya thamani ya bidhaa anayokuwa ameiuza na hivyo akawatajka wafanyabiashara wote kuzingatia.

Alisema fedha zinazokusanywa na serikali kupitia risiti zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu na huduma zingine muhimu za kijamii.

Alisema wanatambua kuwa kuna matatizo mbalimbali yanayotokana na mashine za kutolea risiti za kielektroniki na hivyo huwa wanapita mara kwa mara kuwaelimisha wafanyabiashara ili wasikiuke taratibu.

“Tunapita kwa lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara ili wajitahidi kutoa risiti, tunawaelimisha pia namna ya kufanya wanapobaini kuwa mashine za kutolea risiti zina shida, kwahiyo nawaomba sana watimize sheria ili wasikumbane na adhabu,” alisema Shaban.

Alisema watahakikisha wanafanya ukaguzi kwenye maeneo yote ya mkoa huo ili kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa na uelewa wa kutosha na wanasaidia kuwaelimisha pia wananchi.