FAO yataka wadau kudhibiti magonjwa ya mlipuko nchini

By Rose Jacob , Nipashe
Published at 12:41 PM May 06 2024
Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa wa FAO,  Dk. Elibariki Mwakapeje.
Picha: Maktaba
Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa wa FAO, Dk. Elibariki Mwakapeje.

SHIRIKA la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limewataka wadau nchini kushirikiana elimu juu ya dhana ya Afya Moja kwa jamii ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko nchini.

Rai hiyo ilitolewa juzi jijini hapa na Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa wa FAO,  Dk. Elibariki Mwakapeje wakati wa kikao kazi na wadau wa sekta ya afya. 

“Tumewajengea uwezo viongozi wa ngazi za wilaya, halmashauri za Mkoa wa Mwanza dhidi ya Afya Moja. Suala hili tunalipa kipaumbele kwani kuna maradhi na matatizo wanayowapata binadamu kutokana na vyakula hususani vitokanavyo na mimea na mifugo ambavyo vimekuwa na matumizi makubwa ya dawa,” alisema Dk. Mwakapeje. 

Aliwataka wadau hao  kutumia njia tofauti katika kuielimisha jamii ili kukabiliana na athari zitokanazo na magonjwa hayo. 

Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Moja Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk.Saluum Manyata, alisema kuwa asilimia 60 ya magonjwa yatokanayo na wanyama yanawakumba binadamu. 

Dk. Manyata, alisema  asilimia 75 ni magonjwa mapya,  hali iliyoifanya serikali kukaa pamoja na wadau kuhakikisha wanatatua kupitia sekta ya afya, kilimo na wanyama. 

Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Emily Ngubiagai, alisema dhana hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kisekta, kupambana na matatizo mtambuka yakiwemo ya mlipuko.