KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imeingia makubaliano ya kupeleka marubani wake kufundisha na kusimamia ndege mpya za Airbus A220 za Kampuni ya Ndege ya Ibom iliyopo nchini Nigeria.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kuwa kampuni yake imetoa marubani wake waandamizi wawili.
Matindi, amesema marubani hao watakuwa na jukumu la kuwafundisha kwa vitendo marubani na walimu wa marubani wa Ibom Air kwa muda wa miezi sita.
"Marubani wa ATCL watakuwa na jukumu la kufundisha na kusimamia mafunzo kwa vitendo hadi watakapojiridhisha kuwa marubani wanafunzi na walimu wao wamefikia viwango vinavyotakiwa kurusha ndege hizo," amesema.
Aidha, amesema Ibom Air itailipa ATCL gharama za mafunzo hayo kwa mujibu wa mkataba kwa kipindi chote cha makubaliano.
Amesema makubaliano hayo yamefikiwa baada ya ATCL kuonesha uzoefu wa muda mrefu wa kumiliki ndege za Airbus A220-300 na pia kuridhishwa na kiwango cha umahiri wa marubani wa Air Tanzania.
Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo kwa marubani wa Ibom Air watakaorusha ndege za Airbus A220, ambazo ATCL ina uzoefu wa miaka mingi wa kumiliki ikilinganishwa na Ibom Air ambao ndio wanaanza kutumia ndege za aina hiyo.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya ATCL, ni kuwa na ndege ya mizigo ya Boeing 767-300F ambayo imeanza safari za kwenda nchi mbalimbali ikiwamo Guangzhou China.
Hivi karibuni Matindi amesema kuwa wako kwenye maandalizi ya kuanza safari za kuelekea moja kwa moja London, Uingereza kwa kutumia ndege yake ya Boeing 787-8 Dreamliner.
Pia, amesema wanatarajia kuendelea kuongeza miruko ya kwenda Mumbai, India na Guangzhou, China na kuanzisha safari mpya za Dubai, Muscat, Lagos Nigeria, Kinshasa na Goma Congo DRC.
Akizungumzia huduma mpya ya Air Tanzania App, Matindi, amesema ni huduma inayopatikana kwenye simu za aina zote zinazotumia mifumo ya “android” na zile za “ios”.
Amesema Air Tanzania App inamleta msafiri kwenye ulimwengu halisi wa wasafiri wa anga na kumpa uzoefu wa pekee wa faragha na uhuru wa kuchagua.
“Air Tanzania App sio tu kwa ajili ya kuwezesha safari bali inamwezesha mteja wa Air Tanzania kunufaika na ofa za bidhaa mbalimbali pamoja na kupata huduma za nyongeza,” amesema.
“Kupitia Air Tanzania App, mteja ataweza kuchagua muda wa safari, daraja la safari, kiti, kununua begi la ziada mahali popote alipo, muda wowote anapohitaji kusafiri kwenda sehemu yoyote ndani na nje ya nchi ambapo Air Tanzania inafanya safari zake,” amesema.
Amesema mteja anayetumia Air Tanzania App ataweza kulipia na kupata tiketi yake ya safari papohapo ambapo kwa sasa wateja watapatiwa huduma kwenye vituo 15 vya ndani ya nchi na 11 nje ya nchi.
“Tunakusudia kuongeza vituo vya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea na Musoma na kurudisha safari za Iringa na Mtwara kwa mtandao wa safari za ndani ya nchi ili kuwawezesha wadau wengi kunufuaika na Air Tanzania,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED