KESI ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na kuisababisha serikali hasara ya Sh.milioni 64.2, itaanza kutajwa leo katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha mkoani hapa.
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka tisa ni Amani Mlay, Gerson Mollel na mmiliki wa Kampuni ya Usambazaji Vifaa vya Umeme na Mabomba, Cecy Zumba.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Devotha Msofe. Kwa mujibu wa Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sifael Mshana, mshtakiwa wa kwanza (Mlay), anashtakiwa kwa matumizi mabaya ya nyaraka, kumdanganya mwajiri wake kuhusu dokezo lenye ombi la kiasi hicho cha Sh. milioni 64.2 zinahitajika kwa ajili ya vifaa vya umaliziaji wa ujenzi wa uzio wa Shule ya Msingi Shangarao iliyopo Kata ya Muivaro.
Katika maelezo ya kosa katika nyaraka hiyo ilikuwa ikionyesha Cecy Electrical Plumbing Co. Ltd, iliomba Sh. milioni 64.2.
Katika kosa la pili la matumizi ya nyaraka yenye maelezo ya uongo kutoka kwa Cecy, yakionyesha amewasilisha nyaraka yenye manunuzi ya nondo 500 zenye ukubwa milimita 12 na nondo 500 za milimita 8.
Manunuzi mengine ni malori saba ya kokoto, sita ya mchanga, mifuko 350 ya saruji, matofali 4,000 na wilbaro moja.
Kosa la tatu ni kumdanganya mwajiri wake kuwa Mei 25 mwaka jana kwa kutoa nyaraka ya uongo ya madai ya malipo, ikionyesha anadai Sh. milioni 64.2.
Kosa la nne, ni matumizi mabaya ya nyaraka yenye muhtasari wa kikao cha kamati ya usimamizi wa mradi wa umaliziaji wa ujenzi wa jengo hilo, huku akijua si kweli.
Kosa la tano, linamkabili Cecy Zumba kwa kusaidia kutenda uhalifu, ambapo anadaiwa kutenda kosa kati ya Mei 1 hadi Desemba mwa jana.
Kosa la sita, linamkabili Cecy na Mollel, kumsaidia Mlay kufanya uhalifu kwa kutumia nyaraka za uongo kwa ajili ya kumdanganya mwajiri wake kusaini zilizotokana na kikao.
Kosa la nane, ni wizi kwa watuhumiwa wote, kati ya Mei 1 hadi Desemba mwaka jana.
Vilevile, kosa la tisa linawakabili washtakiwa wote na kuisababishia mamlaka hasara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED