WAKULIMA wa viazi mviringo mkoani hapa wameiomba serikali kuongeza upatikanaji wa mbegu za zao hilo ili kukabiliana na uhaba na kusababisha kushindwa kuzalisha kwa wingi.
Ombi hilo walilitoa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka wakati alipotembelea moja ya shamba la mkulima wa zao hilo lililopo Kijiji cha Mtwango Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Walisema licha ya kuwa mbegu hizo zinauzwa gharama kubwa, upatikanaji wake ni mgumu kutokana na kiwango kinachozalishwa kiwandani bado hakikidhi mahitaji ya wakulima waliopo kwenye vikundi na hata mmoja mmoja.
Walisema kuna wakulima wameanza kulima zaidi ya ekari moja ya zao hilo kutokana na uhaba wa mbegu hizo kwa mwaka huu.
Mmoja wa wakulima hao, Lenard Kadali, alisema msimu wa mwaka ekari moja ya viazi alivuna gunia 136 na kuuza shilingi 65,000 kila moja.
“Changamoto kwa sisi bado inabaki ni mbegu, uhitaji wa sisi wanachama pamoja na wakulima wetu ni kulima zaidi ya hapa, ili kila mtu apate mimi nilime na yule alime inabidi ‘tubalance’ alisema Kadali.
Gladness Charles, alisema hiyo ni mara yake ya pili kulima viazi mviringo, msimu wake wa kwanza alipata gunia 148 kwa ekari na kuuza Shilingi 65,000 kila moja.
“Mwaka jana nililima ekari mbili, mwaka huu imebidi nilime ekari moja kutokana na changamoto ya mbegu ni chache na wakulima tupo wengi,” alisema Charles.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Ushirika Isowelo, Elia Mhonjwa, alisema chama hicho kina wanachama 630 wa zao hilo, eneo waliloomba mwaka huu ni ekari 1,279 na waliomba mbegu tani 700 na kujibiwa watapata tani 400.
Ofisa Kilimo wa Mkoa huo, Wilson Joel alisema mahitaji ya mbegu hizo mkoani humo ni tani 130,000, kati ya hizo zilizopatikana ni tani 400.
“Idadi hiyo ni zile mbegu bora, lakini wapo wakulima wanatumia hizi mbegu za shambani zinazotokana na viazi walivyolima hasa wa huko Makete,” alisema Joel.
Mrajisi wa Mkoa huo, Edmund Massawe, alisema uhaba unatokana na aina ya mbegu ya Sagita kuwa na mwamko mkubwa kwa wakulima hao kwa kuwa imekuwa ikiwapatia faida kubwa wanapoitumia.
“Ukifuatilia hawa Silverland walianza na Isowelo kama mteja wake mkubwa na alikuwa amewalenga wao, lakini msimu huu wameomba tani 700 kwa sasa anapeleka mbegu maeneo mengine kama mikoa Kilimanjaro, Arusha, Iringa na Mbeya kwa hiyo yeye anaangalia kuongeza soko lake,” alisema Massawe.
Akijibu ombi hilo, Mtaka alisema ipo haja ya kuhamasisha watu wengi kuja kuzalisha mbegu za zao hilo mkoani hapa kwa kuwa nchi ina wataalamu wa kutosha wa kilimo.
“Nchi nzima mzalishaji wa mbegu ya viazi mviringo ni mmoja kwa hiyo siku akiamka akakwambia amepoteza interest ya kuzalisha mbegu Tanzania tumekufa,” alisema Mtaka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED