Wakamatwa kwa tuhuma za wizi vifaa vya ujenzi wa shule

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 09:56 AM Jan 21 2025
Mkuu wa Wilaya Gairo, Jabir Makame.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya Gairo, Jabir Makame.

WATU watatu wilayani Gairo, mkoani Morogoro wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi wakituhumiwa kuhusika na wizi wa nondo za ujenzi wa Shule ya Msingi ya Amali katika kijiji cha Kwipipa, kata ya Iyogwe wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Jabir Makame alisema jana kuwa alibaini wizi huo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo katika kata za Iyogwe, Italagwe, Chakwale, Gairo na Rubeho.

Makame aliwataja watuhumiwa hao ni John Mbaluka, Petrol Mauji na Mnyandwa Letema ambao wanadaiwa kujihusisha na wizi wa nondo 10 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Baada ya  kukamatwa, Mkuu wa Wilaya aliagiza Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao uchunguzi utakapokamilika.

"Ninataka polisi mfanye  mahojiano ya kina na uchunguzi, pia kuwahoji watunza stoo na mafundi wote wanaoshukiwa na wizi huo ili kufichua mtandao mzima wa tukio hilo," aliagiza Makame.

Vilevile, Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi wa Kwipipa na Gairo kwa ujumla  kutojihusisha na masuala ya wizi wa vifaa vya miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya wilaya hiyo kwa sababu vifaa hivyo vinanunuliwa kwa fedha zinazotokana na kodi zao.

 "Ninyi wananchi ndiyo mnaopaswa kuwa  na uchungu na mali hizo na ninataka hawa waliokamatwa kuwa fundisho kwa wengine," alisema Makame.

Mkuu wa Wilaya huyo pia aliwaonya makandarasi wababaishaji na wanaochelewesha kukamilisha miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo kuwa hawatavumiliwa na watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuhujumu miradi.

Makame alisema serikali  imetoa  fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta za afya, maji, elimu, barabara na nyinginezo na lengo ni kutatua changamoto za wananchi.

Akizungumzia wizi wa vifaa vya ujenzi wa shule, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwipipa, Herman Mshomi alikiri kutokea wizi huo kijijini kwake, akilaani kitendo hicho cha watu wachache kurudisha nyuma juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema tukio hilo si la kuikomoa Serikali bali ni kujikomoa wananchi wenyewe kwa sababu miradi inayoletwa na serikali hainufaishi serikali, bali wananchi wenyewe na hivyo wanapaswa kuwa walinzi namba moja wa miradi hiyo.