SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii jana iliangazia madhara ya taka hatarishi za hospitalini zinazotapakaa kwenye ufukwe wa Rainbow, Manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam. Endelea kupata undani wa uchafuzi huu wa mazingira...
BAADHI ya vituo vya kutolea huduma za afya vinatupa taka hatarishi za hospitalini kwenye mito na vijito na kuwa chanzo cha uchafuzi wa fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.
Huku kukiwa na sheria zinazoelekeza taratibu maalumu za kuhifadhi, kukusanya, kurejeleza na kuteketeza taka hizo, mikono ya wanaopaswa kuchukua hatua inaonekana kufa ganzi.
Katika ufuatiliaji wake ndani ya Manispaa ya Kinondoni, mwandishi wa habari hii amebaini taka hizo zikishamwagwa katika vijito, husombwa na maji hadi kwenye mito; Mbezi, Feza, Mpiji na Mlalakua inayomwaga maji katika Bahari ya Hindi.
Taka hizo zikishamwagwa baharini na mito hiyo, hukita kwenye fukwe, ukiwamo wa ufukwe wa Rainbow. Bahari haihifadhi uchafu.
Ramadhani Juma mwenye makazi jirani na ufukwe huo, anasema taka hizo hupelekwa baharini na katika mito, hasa mvua kubwa inaponyesha.
Anadai chanzo cha taka hizo ni baadhi ya wamiliki wa vituo vidogo vya kutolea huduma za afya katika manispaa hiyo na maeneo jirani ambao hawafuati utaratibu wa kudhibiti taka hizo, akidai huwalipa fedha kidogo wazoa taka wa mitaani wakazitupe.
"Unakuta mwenye zahanati, kituo cha afya au hospitali anaona kuliko atoe Sh. 50,000 kwa ajili ya kupeleka taka zake sehemu husika, anampa mwendesha mkokoteni Sh. 5000 bila kujali atakwenda kuzitupa wapi. Matokeo yake wanakwenda kuzimwaga kwenye mifereji na mito ambayo huzileta huku kwenye fukwe," Juma anasema.
Maimuna Ally anayefanya biashara ya chakula katika ufukwe wa Rainbow, anashauri serikali iangalie uwezekano wa kudhibiti wanaotupa taka katika Mto Mbezi anaoutaja kuwa ndiyo sababu ya taka nyingi zinazoonekana katika ufukwe huo.
Hawa Abdalah, mwuzaji wa chakula katika ufukwe wa Rainbow, anasema taka hatarishi kwenye ufukwe huo huwa nyingi zaidi mvua kubwa ikinyesha.
"Mabomba ya sindano yanayozagaa katika eneo hili ni hatari kwa sababu mtu akichomwa na hizi sindano, anaweza kupata maambukizi ya magonjwa hatari," Hawa anaeleza uzoefu wake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach A, Mohamed Mzee anasema uchafu huo unatoka kwenye mito, ukiwamo Mto Mbezi.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo anasema wanaendelea kuchunguza kubaini anayetupa taka hizo hatarishi za hospitalini ili wachukue hatua za kisheria.
Mzee anashauri Wizara ya Afya kubana vituo vya kutolea huduma za afya ili zisitupe taka hizo ovyo, hivyo kunusuru afya za watumiaji wa fukwe na viumbe bahari.
"Serikali kupitia maofisa afya ifanye ukaguzi katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya, wavikague na kujiridhisha wapi wanakotupa taka hatarishi za vituo vyao. Itawasaidia kuwabaini wanaotupa ovyo taka hizi.
"Hata sisi viongozi wa mitaa kwa kushirikiana na wajumbe tunapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja kuanza doria ya kuzisaka hospitali zenye tabia hii hatarishi katika mitaa yetu," anasema.
Mmoja wa wabeba taka katika mtaa wa Makani, Anord Magori, anawatupia lawama baadhi ya wabebataka wenzake anaowaita "wenye tamaa ya fedha bila kujali madhara ya vitendo vyao", wanatumiwa na baadhi ya vituo vya afya kutupa kwenye mito taka hatarishi za hospitalini.
"Wamekuwa wanalipwa ujira wa kati ya Sh. 5,000 hadi 10,000 kwa mkupuo mmoja kutegemea na wingi wa taka hizo. Wanatupa taka hizo nyakati za usiku wakihofia kukamatwa na mamlaka za serikali," anadai Magori.
Mwandishi alizungumza na mmoja wa wanaopokea na kutupa taka hizo, mwanamume mkazi wa Kawe, Manispaa ya Kinondoni (jina tunalo). Anasema wanapokea kazi hiyo kwa tahadhari kubwa kwa kuwa wanajua wakikamatwa, adhabu yake ni kubwa ikihusiha kifungo gerezani.
Kama ilivyodokezwa na mtangulizi wake Magori, mbebataka huyo anasema mara nyingi wanakwenda kuchukua taka hizo nyakati za usiku, zikiwa tayari zimefungwa katika mifuko.
"Huwa tunatupa taka za aina hiyo kwa siri nyakati za usiku mnene. Malipo ni Sh. 5,000. Kama mzigo ni mkubwa sana, tunapewa hadi Sh. 10,000. Kuna baadhi ya vituo vya afya wanasubiri mvua ikinyesha wanazisukumizia Mto Msimbazi unaokwenda moja kwa moja baharini," anasema.
Mbebataka huyo ana angalizo lingine kwa mamlaka za kiserikali, kwamba taka hizo hazitoki katika vituo vya kutolea huduma za afya pekee, bali pia hata majumbani ambako kuna wagonjwa wanaohudumiwa wakiwa nyumbani kwa muda mrefu.
Mmoja wa wafanyakazi wa zahanati iliyoko Mbezi Beach, katika Manispaa ya Kinondoni (jina tunalo) anasema sababu kuu ya kuwapa taka hizo wabebataka wa mitaani ni kukwepa gharama alizodai "kubwa".
Mfanyakazi huyo anafafanua vituo hutakiwa kulipa Sh. 3,000 kwa kila kilo ya taka hatarishi katika hospitali za serikali wanakotakiwa kupeleka taka hizo kwa ajili ya kuteketezwa au kurejelezwa.
"Sasa unakuta una kilo 15 inakulazimu utoe Sh. 45,000. Mwenye zahanati anaona kutoa fedha hizo kila wiki ni gharama kubwa, hivyo anakutuma umpe mtu wa mkokoteni Sh. 5000 akazitupe anakojua mwenyewe, lakini huwa tunawaambia kabisa wasitupe kwenye mito iliyopo maeneo ya karibu na zahanati hii," anasema.
Daktari Bingwa Mbobezi wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Maxigama Ndosi, anashauri serikali kutunga sheria kali itakayozuia maduka ya dawa kuuza sindano, isipokuwa kwa wenye kibali cha daktari tu.
Mhandisi kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Boniface Kyaruzi, anasema kuwa mwaka 1999 baraza lilianzisha Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Pwani (TCMP) kwa lengo la kulinda fukwe, mifumo ya mwambao na viumbe hai wa baharini kwa kupambana na uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa mifumo ya ekolojia na kulinda rasilimali za bahari.
Hata hivyo, Kyaruzi anasema kuwa Licha ya NEMC kuanzisha mradi huo, ufukwe wa Rainbow unaendelea kuchafuliwa, hivyo kutoa ishara kwamba mfumo wa utekelezaji sheria una upungufu, huku kukiwa na shida nyingine ya upungufu wa miundombinu ya kuchakata taka.
Anasema NEMC inawajibika kwa mujibu wa kifungu namba 106 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, kinachoitaka kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuhakikisha utekelezaji wa sheria zinazohusiana na mazingira.
Kyaruzi anasema kuwa katika kuhakikisha inadhibiti utupwaji wa taka za hospitalini, serikali ilitengeneza Kanuni za Usimamizi wa Taka Ngumu (2009) zikiwamo taka hatarishi za hospitalini.
"Sheria inaelekeza kuwa uzalishaji taka unapaswa kupunguzwa kadri inavyowezekana kwa kutumia mfumo wa 'Punguza, Tumia Tena na Rejeleza (PTR)' ili kunguza kiasi cha taka kinachopelekwa kwenye madampo," Nyaruzi anasema.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Peter Nsanya, anasema wanatekeleza miongozo iliyowekwa na Wizara ya Afya kwa kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na utaratibu maalumu wa kuchoma taka hizo.
Anataja moja ya mikakati hiyo ni kuhakikisha hospitali na vituo vingine vya afya ambavyo hazina kiteketezi taka, vinaingia mkataba na hospitali zenye kifaa hicho ili kupeleka taka zake huko zikachomwe kwa gharama anazoziita "nafuu".
"Kila baada ya miezi mitatu tunafanya ukaguzi katika hospitali na vituo hivyo kuangalia kama utekelezaji wa agizo hilo unafanyika ipasavyo na wale wanaokiuka kwa mara ya kwanza huwa tunawapa elimu na wakiendelea na tabia hiyo hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao, ikiwamo kufungiwa kituo," anasema.
Mkaguzi wa Mazingira Manispaa ya Kinondoni, Alban Mugyabuso anasema wanayo mikakati mingi ya kukabiliana na utupwaji taka kwenye mito, lakini bado kuna watu wasio waaminifu wamekuwa wanaenenda kinyume cha maelekezo yao.
Anataja mikakati inajumuisha kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kuhusu madhara ya kutupa taka na kuhimiza jamii kutoa taarifa za watu wanaokiuka taratibu za udhibiti wa taka ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkaguzi Mugyabuso pia anasema wanashirikiana na maofisa afya wa manispaa kutoa elimu kwa zahanati, vituo vya afya, hospitali na maduka ya dawa katika manispaa hiyo kuhusu udhibiti wa taka hatarishi za hospitalini.
"Tuwaelekeza hospitali zinazopokea taka hizo na kuzichoma kwa bei rafiki, lakini bado zipo zahanati, vituo vya afya na hospitali zinazokwenda kinyume cha maagizo hayo kwa makusudi.
"Vilevile, kwa kushirikiana na wadau, tunafanya usafi kila mwisho wa mwezi. Wilaya pia imeweka miundombinu ya vidakia taka (trabs) kwenye Mto Feza ili kukamata taka zote kabla hazijaingia kwenye bahari. Ni teknolojia nzuri ambayo itasaidia kukabiliana na uchafuzi wa fukwe," Mugyabuso anasema.
Mwandishi alifunga safari hadi kwenye kiwanda cha Chilambo General Trade Company Limited, kampuni inayojishughulisha na kurejeleza taka na kuteketeza taka za hospitalini kilichoko Kisarawe, mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Gideon Chilamba anasema waliomba kibali cha kuteketeza taka za hospitalini kutoka Wizara ya Afya ili kusogeza huduma hiyo karibu na hospitali za eneo hilo, lakini mwamko wa wahusika bado ni mdogo.
"Tunayo mashine hapa ya kuteketeza taka za hospitalini (incinerator). Tuna leseni ya kupokea taka kutoka hospitali yoyote nchini. Uwezo tulionao ni mkubwa, lakini kazi ni chache sana, mwamko ni mdogo sana. Hata ukiangalia hospitali za hapa (Kisarawe), wengi hawana mashine hii ila sijui wanatupa wapi taka zao.
"Ninafikiri usimamizi duni wa taka za hospitalini ndiyo unasababisha haya. Hata ukienda dampo utakuta taka za hospitalini zimetupwa huko," anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED