Dk. Rweikiza asema CCM imecheza kama Pele

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 AM Jan 21 2025
Dk. Rweikiza asema CCM imecheza kama Pele.
Picha: Mtandao
Dk. Rweikiza asema CCM imecheza kama Pele.

MBUNGE wa Bukoba Vijijini (CCM), Dk. Jasson Rweikiza amesema hatua ya chama chake kumteua mapema Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na na Dk Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar ni sawa na kucheza kama Pele. (mchezaji mpira wa zamani wa Brazil aliyepata mafanikio makubwa kisoka).

 Akizungumza na Nipashe Digital hili leo  Dk. Rweikiza amesema Rais Samia anastahili miaka mitano tena kwa uchapakazi wake uliosababisha kukamilika kwa miradi yote ya kimkakati ikiwemo ya reli ya mwendokasi SGR na bwawa  la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

Dk. Rweikiza pia amepongeza uteuzi wa Rais Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa urais Zanzibar kwani ndani ya miaka michache ya uongozi wake amefanya mambo makubwa ambayo yanamfanya kustahili mitano tena.

Amepongeza pia uteuzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi  katika nafasi ya mgombea mwenza kuwa ni turufu nyingine kwa CCM kwani ni mtu mwenye uzoefu wa kutosha, mwadilifu, mzalendo wa kweli na asiye na makuu.

“Nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumleta Dk. Nchimbi  kuwa Makamu wa Rais kwasababu ni  mtu ambaye uadilifu wake hauna mashaka kabisa… CCM imepanga safu bora kabisa nampongeza pia Makamu Mwenyekiti mteule ndugu Steven Wasira ambaye uzoefu wake ndani ya chama na serikali unaonekana dhahiri,” amesema

“Ndani ya muda mfupi ambao Dk. Nchimbi amekuwa Katibu Mkuu wa chama tumeshuhudia mageuzi makubwa sana ndani ya chama nampongeza sana Rais Samia kwa kumteua maana ni mtu mzoefu na mwadilifu sana,” amesema Dk Rweikiza