RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia watanzania na jumuiya za kimataifa kuwa Tanzania ni eneo salama licha ya kubainika kisa kimoja cha mtu aliyeambukizwa virusi vya ugonjwa wa Marburg wilayani Biharamuro, mkoani Kagera.
Amesema hatua zilizochukuliwa mwaka 2023 kudhibiti virusi hivyo wakati vilipobainika nchini, zimeiwezesha Tanzania kuwa na uzoefu wa kutosha kudhibiti maambukizi.
Rais Samia aliyasema hayo jana Ikulu ya Chamwino, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tedros Ghebreyesus.
"Serikali ilituma timu ya wataalamu Januari 11 mwaka huu, kuchunguza kuhusu ugonjwa huo ambapo katika sampuli zilizochukuliwa, mgonjwa mmoja pekee ndiye aliyekutwa ameambukizwa," alisema.
Rais alisema hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwamo kufanya uchunguzi kwa kufanya kazi karibu na mamlaka za serikali za mitaa, kuanzisha kikosi kazi cha dharura, kupeleka timu ya uchunguzi kufanya tathmini ya hali halisi kisha kutoa taarifa kwa umma.
Dk. Ghebreyesus alisema kuwa kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Tanzania katika kudhibiti maambukizi hayo, WHO imetoa dola za Marekani milioni tatu kuongeza nguvu katika mapambano hayo.
Alisema Tanzania ina uzoefu wa kutosha kukabiliana na maambukizi hayo na ndiyo sababu WHO inaunga mkono juhudi za serikali.
Dk. Ghebreyesus pia alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itatoa hakikisho kwa wananchi kupata huduma za afya kwa uhakika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED