WAFANYAKAZI wa Kiwanda cha chai cha DL Kibena wameingia siku ya saba kwenye mgomo wa kuingia kazini kwa madai ya kushinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara ya miezi minne.
Wakizungumza na waandishi wa habari, nje ya kiwanda hicho, walidai uongozi wao haujawalipa mishahara yao kwa kipindi hicho na kushindwa kumudu gharama za maisha.
Mmoja wa Wafanyakazi hao, Chesco Mligo, aliiomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha wanalipwa mishahara hiyo ili wamudu kuendesha maisha yao.
“Tunazungumza hili kwa uchungu kwa sababu tangu huyu mwekezaji amefika sisi ni watu wa kulia tu licha ya kumpandia chai na biashara anafanya,” alidai Mligo.
Kalorina Komba, alidai kutolipwa mishahara hiyo kumesababisha washindwe kumudu mahitaji ya familia kwa kukosa fedha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Mashambani nchini (TPAU) Tawi la kiwanda hicho, Elisha Mbembati, alisema kuwa mwajiri huyo amelipa mshahara wa mwezi mmoja na kuwaomba wafanyakazi hao kurejea kazini na kuahidi kuendelea kulipa.
Katibu wa TPAU wa tawi hilo, Frida Kidenya alisema mwajiri huyo pia hajawasilisha michango ya wafanyakazi kwenye Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa muda wa miaka sita.
Meneja wa Kiwanda hicho, Geradi Ng'enzi, alithibitisha wafanyakazi hao kudai malimbikizo hayo ya mishahara na kuahidi kuendelea kulipa kadri fedha zitakapo patikana walau kwa mwezi mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED