RC Macha kuzindua maadhimisho Wiki ya Sheria

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:51 PM Jan 20 2025
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali.
Picha: Marco Maduhu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Januari 25, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, katika viwanja vya Zimamoto vilivyopo Manispaa ya Shinyanga. Wiki hiyo ya sheria itahitimishwa Februari 1, 2025, katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Shinyanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali, akizungumza na vyombo vya habari leo, Januari 20, 2025, amesema maadhimisho haya yanaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka mpya wa kisheria, baada ya likizo ya Mahakama inayomalizika Januari 31 kila mwaka.

Katika maadhimisho hayo, utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi utaboreshwa kwa kutumia utaratibu wa kuwafikia moja kwa moja katika maeneo yao. Jaji Mahimbali amefafanua kuwa, kutokana na wananchi wengi kuwa kwenye shughuli za kiuchumi wakati wa wiki za kazi, elimu ya sheria mwaka huu itatolewa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu kwa kutumia magari maalum yatakayozunguka kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Elimu hii ya kisheria pia itawafikia wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, na vyuo, huku tukiongeza wigo kupitia vyombo vya habari kama luninga, redio, na mitandao ya kijamii,” amebainisha Jaji Mahimbali.

1

Aidha, maadhimisho hayo yatahimizwa na bonanza kubwa la michezo litakaloshirikisha watumishi wa Mahakama kutoka ukanda huo, ili kukuza mshikamano na ushirikiano.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinasosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Jaji Mahimbali amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya Mahakama na taasisi nyingine za utoaji haki katika kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa, ikilenga kufikia uchumi wa kiwango cha kati wa ngazi ya juu ifikapo 2050.

Ameongeza kuwa Mahakama imejipanga kutekeleza dira hiyo kwa maboresho ya utendaji kazi, kuhakikisha utoaji wa haki kwa wakati, na kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria nchini.

2