CCM yawapitisha Samia na Mwinyi kuwania urais 2025

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:30 AM Jan 20 2025
CCM yawapitisha Samia na Mwinyi kuwania urais 2025.
Picha: CCM
CCM yawapitisha Samia na Mwinyi kuwania urais 2025.

VIJANA wa mitaani wana kauli yao "imeisha hiyo" wakiwa na maana ya kuwa na uhakika wa kutimia kwa jambo lao. Wajumbe wa vikao vya juu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nao wameshakamilisha mapema.

Hii ni baada ya ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kupitisha azimio kuwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar kuwa wagombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wajumbe wa mkutano huo walifikia hatua hiyo jana baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ambayo ilionesha chini ya uongozi wao wametekeleza miradi ya maendeleo na ya kimkakati vizuri na inawagusa wananchi.

Akisoma azimio hilo, Mjumbe na Mbunge wa Viti Maalumu, Ng’wasi Kamani, alisema kwa kuzingatia mamlaka waliyonayo wajumbe chini ya Ibara ya 101(5)(b) ya Katiba ya CCM, wanaazimia jina la Samia kuwa ndiye mwanachama atakayesimama kugombea kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, alisema chini ya Ibara ya 103(c) ya Katiba hiyo, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ndio yenye mamlaka ya kuchagua jina moja la wanachama atakayesimama kugombea urais wa Zanzibar na jana walielekeza NEC kukutana kutekeleza jukumu hilo la kumchagua Mwinyi kuwa mgombea wa urais Zanzibar.

Kabla ya kufikiwa hatua hiyo, kutokana na hoja za wajumbe, Rais Samia alisema anaogopa kuzungumza na kuomba ushauri kwa viongozi wastaafu kama jambo hilo linawezekana.  

Akifafanua kuhusu hilo, Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, alisema kila chama kina utaratibu wake wa kuteua wagombea na uamuzi ni wa kikao hicho na kwamba kuna nchi kama Namibia wanafanya uamuzi wa wagombea mwaka mzima.

"Kama tunataka kuamua leo (jana) Samia na Mwinyi ni wagombea wetu, mamlaka hayo tunayo. Kama tunaamua hivyo ndio tumeamua, kilichobaki ni ushauri wa wale wanaojua taratibu za sheria, lakini watu wote watajua tu kuwa CCM kwenye uteuzi wa wagombea imemaliza," alisema.

Alisema kazi kubwa imefanywa na viongozi hao kupitia taarifa ya utekelezaji ilani iliyowasilishwa kwenye mkutano huo, imeonesha wana-CCM hawakukosea kwa kuwa ni watu makini, wanajua wanachofanya na kinachotakiwa kufanyika.

"Ushindi wa CCM ni dhahiri, ushindi kwa mwaka huu hauna mjadala, wagombea watakuwapo wa vyama vingine lakini sioni namna wanavyoweza kuishinda CCM, lakini si kwa ujanjaujanja, yapo mambo mengi mazuri yaliyofanywa na serikali zetu na yana manufaa kwa watanzania.

"Mnaweza kufanya mambo mengi mazuri lakini hayajawagusa watanzania. Haya yanagusa maisha," Kikwete alisema.

Aliongeza kuwa wananchi watatambua na kuthamini kazi iliyofanywa na viongozi hao na kushauri wana-CCM wasibweteke.

"Siku zote jipe rai kwamba uchaguzi huu utakuwa mgumu. Hiyo ndio falsafa ya jeshi, maandalizi yetu yawe kwamba tunakwenda kwenye vita kubwa na si ndogo na tujiandae kwamba tunakwenda kwenye mapambano makubwa.

"Lazima tujiandae vizuri, na mimi niliyoyasikia hapa, bwana aah! Sijui labda kutokee mchawi na wachawi walishakufa, hawapo tena," alisema.

Kikwete alisema wajumbe wa mkutano wanamtaka Samia na Mwinyi waendelee na kwamba hakuna wa kusema 'hapana'.

"Namna ya kulifanya jambo hili, liandaliwe azimio maalumu la mkutano ili kutamka, liletwe na ithibitishwe na linakubaliwa na inakuwa sasa rasmi uamuzi wa mkutano mkuu," alisema.

Mwenyekiti mstaafu huyo pia aliwaomba viongozi na wajumbe kuwaeleza wanachama na wananchi yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia na Mwinyi na sababu ya kuwapitisha kuwapa ridhaa tena.

Vilevile, alimpongeza Katibu Mkuu Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kwa utendaji wake mzuri huku akieleza kuwa Makamu Mwenyekiti mpya, Stephen Wasira anajulikana kwa uwezo wake wa uongozi, kupambana na kujenga hoja, hivyo nafasi hiyo imepata mtu madhubuti.

Alisema mkutano huo umemwonesha sura ya CCM anayoijua kwa kuwa mikutano mikuu ndio inaonesha nguvu ya kuendelea mbele na hana shaka wajumbe watarudi na nguvu mpya.

Baada ya ufafanuzi huo, Mwenyekiti Samia alielekeza Sekretarieti ya CCM Taifa ikaandae azimio hilo na kupeleka kwenye mkutano huo.

Awali, miongoni mwa wajumbe waliozungumzia suala hilo ni Mbunge wa Mvumi na Mjumbe wa Mkutano Mkuu, Livingstone Lusinde, aliyesema ilani imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100 na kwamba hakuna deni, wananchi wameona yaliyofanyika kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu.

Alisema mkutano huo ni mkubwa na wenye uamuzi, hivyo akaomba wajumbe wafanye uamuzi ili mwenyekiti aone uzito wa mkutano huo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa alisema wajumbe wameshuhudia miradi iliyotekelezwa na hakuna ambaye hajaguswa na kuomba wajumbe waazimie kuwapitisha Samia na Mwinyi wawe wagombea wa nafasi ya urais.

Kwa kupitishwa huko, Samia atakuwa mgombea urais wa kwanza mwanamke kupitia CCM tangu Uchaguzi Mkuu wa kwanza nchini mwaka 1995.