MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo, Frank Mbosa, amepongeza juhudi za chama chake katika kuongeza idadi ya wanachama watakaoshiriki zoezi la upigaji kura za maoni kwenye mchakato wa ndani wa kutafuta wagombea wa ubunge na udiwani.
Mbosa ametoa pongezi hizo leo, Januari 20, wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa habari, ambapo amewasihi viongozi wa ngazi mbalimbali za chama, kuanzia mashina, matawi, kata hadi wilaya, kuhakikisha wanaandaa mipango madhubuti ya kusimamia na kushirikisha wapiga kura wapya pindi muda wa zoezi hilo utakapowadia.
“Bila uratibu mzuri wa utaratibu huu, ongezeko la wanachama linaweza kusababisha vurugu na kuwa chanzo cha migogoro ndani ya chama,” alionya Mbosa, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa.
Aidha, Mbosa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa uongozi wao mahiri. Alisisitiza kuwa utendaji wao umeimarisha imani ya chama na kuongeza kuwa, ana hakika CCM itaendelea kushinda kwa kishindo katika chaguzi zijazo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED