WATUMIAJI fukwe zilizo karibu na mito inayomwaga maji Bahari ya Hindi katika Manispaa ya Kinondoni, mkoa wa Dar es Salaam, wako hatarini kukumbwa na maradhi kama vile saratani, tetenasi na kuambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU), imebainika.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii, umebaini baadhi ya fukwe katika manispaa hiyo zina taka hatarishi za hospitalini zinazomwagwa katika mito inayomwaga maji baharini.
Hatua hiyo inakinzana na maelekezo yaliyomo katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 ambayo katika vifungu vya 137 na 139 inaelekeza kuwapo utaratibu maalumu wa kuhifadhi taka hatarishi, zikiwamo za hospitalini.
Sheria hii pia inawapa jukumu Waziri wa Afya na yule mwenye dhamana ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha taka hizo zinachambuliwa na kutunzwa katika kontena maalumu na kuteketezwa kwa utaratibu maalumu.
Mwandishi amebaini utekelezaji wa maelekezo hayo ya kisheria ni hafifu, hivyo kusababisha utupwaji taka ovyo mitaani ambazo baadaye huishia kwenye vyanzo vya maji, zikiwamo fukwe za Bahari ya Hindi, mkoani Dar es Salaam.
Taarifa ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyochapishwa mwaka 2019, inabainisha kuwa mkoa huo huzalisha taka ngumu, zikiwamo za hospitalini, tani 4,600 kwa siku.
Hata hivyo, taarifa hiyo inabainisha kuwa ni asilimia 6.5 (tani 299) tu ndiyo hurejelezwa, hivyo kuziacha tani 4,301 (asilimia 93.5) zikitupwa ovyo mitaani, ikiwamo mito na hatimaye kuishia kwenye fukwe za bahari.
Vilevile, utafiti uliofanywa na S.V. Manyele (ACHA UZEMBE, SEMA S.V NI NANI?) na wenzake mwaka 2013, ukitathmini mifumo ya usimamizi wa taka za hospitalini katika vituo vya afya vya ngazi za chini (LLHF) katika wilaya za Ilala na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, ulionesha kuwa asilimia 83 ya vituo vya kutolea huduma za afya katika Manispaa ya Kinondoni hufukia taka katika mashimo.
Watafiti hao pia walibaini lingine la ziada, kwamba zaidi ya asilimia 50 ya maeneo ya wanakotupa taka hizo hayakuwa na uzio na yalikuwa karibu na makazi ya watu.
"Asilimia 47 ya vituo vya afya katika wilaya za Ilala na Kinondoni hazina taratibu za uendeshaji wa kawaida wa usafirishaji taka za hospitalini.
"Ni changamoto kubwa zaidi katika Manispaa ya Kinondoni ambako asilimia 71 ya vituo vya afya hubeba taka hatarishi kwa mikono wakati wa kwenda kuzitupa, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Mazingira," inasomeka sehemu ya ripoti ya watafiti hao.
Licha ya angalizo hilo la miaka 12 iliyopita, mwandishi wa habari hii amefika kwenye ufukwe wa Raibow, katika Manispaa ya Kinondoni na kukuta taka hatarishi, zikiwamo za hospitalini, zikiwa zimetapakaa pembezoni mwa ufukwe.
Hizo zinajumuisha mabomba ya sindano, dripu, mifuko ya kuwekea dawa na chupa za dawa ambazo baadhi zilionesha muda wa matumizi yake umeshapita, hivyo kuwaweka hatarini kiafya watumiaji wa eneo hilo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), Sarah Pima anasema kuwa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira, huwa wanafanya usafi katika ufukwe huo mara mbili kwa mwezi, wakikusanya taka, kuzitenga na kuzirejeleza.
Sara anabainisha kuwa kila wanaposafisha ufukwe huo, hukusanya wastani wa tani nne hadi 13 za taka ngumu. Kati yake, asilimia nane ni taka hatarishi za hospitalini.
"Kinachotusikitisha kila tunaporudi kusafisha ufukwe (kila baada ya wiki mbili), tunakuta kiwango kikubwa cha taka kana kwamba hakujafanyiwa usafi kwa muda mrefu," Sara anasema.
Ramadhani Juma anayejitambulisha ni makazi jirani na ufukwe huo, anasema hali ya uchafu katika ufukwe huo imekuwa mbaya zaidi kulinganisha na miaka mitano iliyopita.
"Miaka mitano iliyopita eneo hili lote lilikuwa safi, watu walikuwa wanajaa hapa hadi saa sita za usiku, lakini siku hizi watu wahesabika, wakizidi sana ni 20. Mandhari imeharibika, watu wanahofia afya zao kama wakikanyaga mabomba ya sindano si wanaweza hata kuambukizwa hata VVU?" Juma analalamika.
Mfanyabiashara wa vinywaji katika ufukwe wa Rainbow, Ramadhani Ally anasema uchafu huo umesababisha biashara kuzorota, akifafanua kuwa watu waliokuwa wanakwenda kutembelea na kupunga upepo ufukweni huko wamepungua kutokana na hali hiyo iliyoelezwa na mtangulizi wake Juma.
Anasimulia kuwa awali alikuwa anafanya biashara hadi saa nane usiku kwa kuwa eneo hilo lilikuwa safi na lenye watu wengi, lakini hivi sasa anafunga biashara saa mbili usiku kwa kuwa giza likiingia, watu wanaondoka wakihofia kukanyaga taka na kudhuru afya zao.
"Miaka mitano ya nyuma hapa nilikuwa ninaingiza hadi Sh. 300,000 kwa siku, na duka langu lilikuwa kubwa kuliko lilivyo hivi sasa, lilikuwa limejaa vinywaji, lakini sasa nikiuza sana ni Sh. 50,000 kwa siku.
"Kama unavyoona, duka halina kitu maana hata ukijaza vinywaji vitaisha muda wake wa matumizi vikiwa dukani, unapate hasara, hakuna wanywaji," Ally anasema.
Maimuna Ally anayefanya biashara ya chakula katika ufukwe huo, anasema "kuwapo taka hizi zinazotoa harufu mbaya, ni sababu kuu ya wateja kutukimbia. Biashara yangu imeathiriwa sana. Yaani ninaambulia Sh. 30,000 kwa siku ilhali zamani nilikuwa ninatoka Sh. 100,000 kipindi ambacho ufukwe ulikuwa safi."
Hawa Abdallah naye ana biashara ya chakula katika ufukwe huo. Anasema biashara imekuwa ngumu kutokana na ufukwe kuwa na harufu mbaya aliyoifananisha na harufu ya msalani.
"Yaani ni kama tuko... (anatamka neno lenye maana ya msalani). Upepo ukivuma harufu inasambaa, hali inakuwa mbaya zaidi kwenye eneo hili.
"Si taka za hospitalini tu, bali watu pia huwa wanavizia mvua ikianza kunyesha, wanafungulia mabomba ya vyoo na kutiririsha maji taka. Kama inavyofahamika bahari haikai na uchafu, hivyo madhara yake lazima yanatukumba sisi tuliopo hapa ufukweni," Hawa analalamika.
Daktari Bingwa Mbobezi wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Maxigama Ndosi anasema taka hizo zinaweza kusababisha madhara kwa watumiaji fukwe, ikiwa ni pamoja na kuambukizwa magonjwa hatari kutoka kwa wanyama au wadudu kwa njia ya damu.
Anasema kuwa kama sindano ina kutu, kunakuwa na uwezekano mkubwa mtu kupata tetenasi. Katika hili la kutu, Bingwa Mbobezi Ndosi anatoa angalizo kwamba, kati ya wagonjwa 10 wa tetenasi, sita hufariki dunia.
Bingwa Mboezi Ndosi Alisema sindano hizo hazitupwi na zahanati pekee bali hata watu binafsi baada ya kuzitumia na kuishauri serikali kuweka sheria ngumu kuzuia maduka ya dawa yasiuze sindano kwa wato ovyo bali wale wenye kibali cha daktari.
Dk. Ndosi anasema miongozo inaelekeza taka hatarishi zibebwe katika vyombo maalumu vilivyoandika taka hatarishi na huwa hazitupwi kama taka za kawaida, bali zina utaratibu wake maalumu wa kuzikusanya na kuzitekeleza.
"Hata vyombo vyake vya kuzihifadhi huwa vina rangi ambazo zinaonesha ni taka hatarishi ambazo hazipaswi kuhifadhiwa kwa namna ya kawaida," Bingwa Mbobezi Ndosi anasema.
Profesa Philip Bwathondi wa Shule ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi (SOAF) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema taka hizo zinapotupwa baharini, zinaweza kusababisha madhara kwa viumbe wa baharini kama vile vidonda kwa samaki pale sindano zinapowachoma.
"Athari hizo zipo pia kwa binadamu kwa sababu maradhi yake huwa yaniangia mpaka kwa mlaji wa mwisho ambaye ni binadamu.
"Wadudu wengine wanabeba vimelea kutoka katika hizo taka na mlaji wa mwisho ni binadamu. Katika kila hatua vinapenya mpaka vinafika katika mwili wa binadamu na hatimaye kusababisha maradhi kama vile saratani," anafafanua Prof. Bwathondi.
*USIKOSE KUFUATILIA KESHO KUJUA ZINAKOTOKA TAKA HATARISHI ZA HOSPITALINI ZINAZOTAPAKAA UFUKWENI
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED