NAIBU Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mcha Hassan amesema Mkoa wa kikodi Kariakoo katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25 umekusanya Sh. bilioni 71 .7 kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza sawa na ufanisi wa asilimia 104.
Mcha alisema hayo jana wakati wa bonanza la kuelekea kilele cha mlipakodi Januari 23 mwaka huu, lililoandaliwa na TRA Mkoa wa Kikodi Kariakoo kwenye viwanja vya Jakaya.
Alisema Kariakoo ni mkoa wa kikodi wa kimkakati na kwamba umefanikiwa kukusanya kiwango hicho kutokana na kusogeza huduma muhimu kwa wafanyabiashara 30,000 wanaotegemea soko hilo.
"Kama tunavyojua, soko hili linategemewa na watu kutoka Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Visiwa vya Comoro," alisema.
Mcha alisema kwa mwaka huu Kariakoo itaendelea kuwa kiungo muhimu pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kwenye matukio ya pamoja ili kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya sekta binafsi na mamlaka hiyo.
Aliwashukuru wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari kukuza Pato la Taifa na kuwaahidi kuendelea kufanya nao kazi kwa weledi na ubunifu kupitia mikakati yote waliyoweka.
Alisema wataendelea kuongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, kuongeza huduma mashine za kielektroniki kwenye sekta hiyo.
"Tumekuwa tukiweka mikakati mingi ambayo mingine inalenga kuwasaidia wafanyabiashara wote na hawa si wa ndani tu, hata wengine wanaotoka nje ya nchi, na tutaendelea pia kusisitiza watu walipe kodi kwa hiari ili kuepuka changamoto ndogondogo," alisema Mcha.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severin Mushi alisema kuwa kwa sasa wafanyabiashara wako tayari kulipa kodi kwa hiari na hayo ni matunda ya mikutano iliyofanyika kati yao na TRA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED