Pinda asilimulia tamu na chungu mitandao kijamii

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:17 AM Jan 19 2025
 MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,  Mizengo Pinda.
Picha:Mtandao
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Mizengo Pinda.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Mizengo Pinda, ameeleza mitandao ya kijamii ilivyomtoa jasho.

Akizungumza jana jijini hapa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, Pinda ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, alisema kuelekea mkutano huo hasa kujazwa kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, mitandao hiyo ilikuwa pasua kichwa. 

Pinda alipewa nafasi hiyo baada ya jina la mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira, kutajwa kuwa ndiye amependekezwa kuziba nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana. 

“Mitandao hii wakati mwingine inakutoa jasho. Ukigeuka  huku kuko hivi ukigeuka huku, unafika mahali unafikiria labda kuna mmoja amenong’onezwa kwamba mzee unakuja kuwa makamu kumbe wapi, kumbe sivyo,” alisema. 

Alisema juzi alipata nafasi ya kwenda Zanzibar na kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mmoja wa watu waliokuwa wamepewa jukumu la kwenda kusimamia uchaguzi kwenye nchi zilizo chini ya Jumuiya na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Pinda alisema  yeye alikuwa wa kwanza kuingia na baada ya kumaliza kumsimulia aliyotekeleza, mwishoni alibaki anasubiri labda kama Rais Samia atasema neno kuhusu umakamu.

“Nikawa sioni dalili kama mitandao inavyoeneza nikasema ameniweka nini? Lakini haikufanyika hivyo mwishoni nikasema mmmh huyu mama mmh lakini kumbe ni utaratibu tu. Unataka  akwambie siri halafu utoke uanze kuropoka? Lakini  nikasema angalau nimempa ujumbe na baada ya kutoka hapo na kurudi, mitandaoni wakaona nimepiga picha nipo na nani wakasema ameitwa huko. Nikasema  mngejua lakini yakaisha vizuri na ninashukuru jambo hili sasa limefikia tamati.

“Najua wote waliokuwa wakisema sema huko ni kwa nia nzuri lakini tukifikia hatua hii tunaingia kwenye kazi ya Chama cha Mapinduzi na tunakijenga kwa kuonesha mshikamano na tutaonesha katika zoezi hili la kumpata Makamu Mwenyekiti lazima nikubali chama changu ndio hasa hazina tunayoitafuta,”alisema.

Kadhalika, alisema miaka 17 iliyopita baada ya Hayati Edward Lowassa kuacha madaraka ya uwaziri mkuu, mitandao iliibuka na hisia zake ikiimtaja yeye na Wasira kushika nafasi hiyo na sasa tena limetokea hilo.

Alisema amekaa na Wasira na wamefanya kazi kwa pamoja na yaliyotokea si usumbufu kwake na ataendeleza hali ya mshikamano hata kwenye mazingira hayo. 

“Mimi namjua Wasira kama kada mmoja mahiri sana kwenye chama chetu na nilipokuja kusoma kahistoria kake nikashtuka nikasema eeh! huyu mzee kumbe sivyo kama nilivyokuwa namfikiria. Ameibukia  kumbe kwenye TANU enzi hizo mwaka 1959 amepata kadi ya uanachama akiwa na miaka 16. 

“Amekuwa kwenye nafasi mbalimbali ni libaba ana uwezo mkubwa sana kichama na shughuli za serikali kwa ujumla,” alisema 

Alisema hana shaka na uwezo wa Wasira hata kidogo kwa kuwa wamefanya kazi kwa karibu na kuna wakati kulipokuwa na matatizo kwenye mikoa alikuwa akishauri apelekwe Wasira kwenda kuyamaliza na hadi leo anaenziwa kwa mengi.