Timu ya Mbowe yashusha takwimu za mafanikio

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:56 AM Jan 19 2025
Mratibu wa kampeni za Mbowe, Daniel Naftali.
Picha: Mtandao
Mratibu wa kampeni za Mbowe, Daniel Naftali.

TIMU ya kampeni ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, imeshusha takwimu za mafanikio kwa miaka 21 ambayo amekiongoza chama hicho.

Aidha, imeahidi kwamba uchaguzi mkuu wa chama hicho utafanyika mubashara kuanzia wakati wa wagombea kuomba kura, kupiga na kuhesabu kura hadi kutangaza matokeo, ili kuhakikisha kila hatua, inakuwa ya uwazi na haki.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu wa kampeni za Mbowe, Daniel Naftali, alisema anaamini Mbowe atashinda kwa kishindo kwa kuwa historia ya kukijenga chama hicho inaonekana wazi na inambeba

Alisema wanaamini Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anayewania kukalia kiti cha Mbowe, anafaa japokuwa akilinganishwa na Mbowe, anapungua.

“Hatusemi Lissu hafai. Sisi  tunasema anafaa ila ukimlinganisha na Mbowe, anapungua. Tunachojadili ndani ya chama ni tofauti na minyukano inayoendelea kwenye mitandao. Umma una wajibu wa kutoa maoni yao. Sisi  CHADEMA tuna haki ya kuchagua kiongozi tunayeona anafaa,” alisema.

Alisema keshokutwa uchaguzi wa kuamua nani aiongoze CHADEMA kati ya Lissu na Mbowe utakuwa mubashara ili wananchi wote washuhudie.

Alisema CHADEMA imefikia kutengeneza mjadala nchini kwa sababu ya uongozi makini wa Mbowe kukuza taasisi.

TAKWIMU

Alisema katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 baada ya Mbowe kuanza kuongoza CHADEMA, chama hicho kilipata wabunge 11 na madiwani 102.

“Uchaguzi wa mwaka 2010, CHADEMA ilipata wabunge 49 na madiwani 572 na mwaka 2015 CHADEMA ilipata wabunge 72, madiwani 1,108 na halmashauri 23. Hizi ni takwimu ambazo zinaonesha chama kinapaa. 

“Mbowe amekipatia chama mafanikio yanayoshikika. Alisema Mbowe aliingia madarakani chama hicho kikiwa kidogo nchini na kwamba chini ya uongozi wake, kimekuwa chama kikuu cha upinzani.

Naftali alisema uwezo mkubwa wa Mbowe unavitisha vyama vingine, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kinaogopa ushindani wa haki kwenye sanduku la kura.

“Tunaamini mheshimiwa Mbowe anayo nguvu ya kukipeleka chama mbele zaidi,” alisema.

Mbali na takwimu za uongozi, Naftali alisema Mbowe anaungwa mkono na wenyeviti wa CHADEMA mikoa 17 na wanane wa Kanda.

“Siasa si kutuhumu wenzako mambo ya uongo bali ni hoja. CHADEMA unayoiona kila mtu ana mchango wake, ana tofali lake. Wengi wetu tumefungwa na hata akina Lissu. Ndio maana kila mwanachama ana mchango wa pekee kuifanya CHADEMA iwe hivi ilivyo,” alisema.

Kuhusu tuhuma za Lissu kwamba timu ya kampeni ya Mbowe inagawa rushwa kwa wajumbe, alisema  sio za kweli na kwamba hazina uthibitisho wowote.

“Kama kuna mtu anaushahidi wa mimi kutoa rushwa sehemu yoyote. Niko  tayari kuwajibika. Kabla sijawa mratibu wa kampeni za Mbowe, mimi ndiye niliyemfanyia kampeni Lissu, nilimchukulia fomu, nikaijaza, nikamtafutia kura na akashinda akiwa Ubelgiji,” alisema.

Alisema Lissu ameibua tuhuma za rushwa kwa kuwa (Naftali) amekuwa upande wa Mbowe. 

Mratibu huyo alisema wakati huu wa kampeni za ndani ya chama, kumejengeka tabia ya baadhi wa wagombea kudhani wao ni wasafi kama Malaika na wengine ni wachafu kama shetani.

“Wanataka kujipa umalaika, wanataka jamii iamini kwamba kumuunga mkono Mbowe sio sawa, ila kumuunga mkono Lissu ndio sawa,” alisema.

VIPAUMBELE

Naftali alisema kipaumbele cha kwanza kama Mbowe atashinda ni kuhamasisha vuguvugu la mchakato wa Katiba Mpya na kwamba ili kuipata, wameandaa mkakati wa kuunganisha makundi yote ndani ya jamii.

Alisema lengo ni kupata Katiba Mpya kwa nguvu kubwa ya umma.

Lingine ni kuunda tume ya ukweli na maridhiano, itakayofanyakazi ya kuondoa mgawanyiko ndani ya chama hicho, ambao umesababishwa na uchaguzi.

“Tunajua tumegawanyika na hili halikwepeki kwenye demokrasia. Tume itaunganisha wanachama ili turudi kuwa familia moja,” alisema.

Alisema jambo hilo litafanywa sambamba na kurudisha chama ngazi ya vitongoji na matawini, ili kuhakikisha kinakuwa na mizizi kuanzia ngazi ya chini.

Kipaumbele kingine, alisema ni kuwasaidia wagombea wa CHADEMA katika ngazi mbalimbali kwa kuwawezesha kushindana na wapinzani wao mbele ya umma, kirasilimali na mambo mengine.

Alisema kipaumbele kingine ni kuendeleza programu maalum ya elimu ya uraia, ili vijana wanaochipukia kwenye siasa wafahamu msingi na umuhimu wa kuendeleza demokrasia ya vyama vingi.

Uchaguzi Mkuu wa CHADEMA umepangwa kufanyika Dar es Salaam Januari 21, 2025 ambapo nafasi ya Uenyekiti inawaniwa na Mbowe, Lissu na Charles Odero, wakati John Heche na Ezekia Wenje, wakichuana kurithi mikoba ya Lissu kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa.