JKT Tanzania yasitisha likizo za wachezaji wake

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:16 AM Jan 19 2025
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally

BAADA ya Bodi ya Ligi kutoa tamko la kuanza tena Ligi Kuu mwanzoni mwa mwezi ujao, Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesitisha likizo za wachezaji wake akiwataka haraka kambini kwa ajili ya kujiandaa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kocha huyo alisema anawarudisha haraka wachezaji wake mazoezini kwa kuwa muda siyo rafiki baada ya kuahirishwa kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN),  zilizotarajiwa kuchezwa kuanzia Februari Mosi hadi 28, mwaka huu, lakini zimesogezwa mbele mpaka Agosti mwaka huu.

"Tulijua ligi itarejea mwezi Machi kama tulivyotangaziwa awali, ndiyo maana wachezaji walikuwa likizo na ilikuwa inaendelea, sasa baada ya kuahirishwa ligi imerudishwa nyuma, tunatakiwa haraka tukutane tuanze matayarisho kwa sababu muda sasa ni mfupi kuliko mwanzo," alisema kocha huyo.

Kutokana na hilo, wachezaji wa JKT Tanzania walitarajiwa kuanza mazoezi jana jioni baada ya likizo zao kukatishwa.

Pamoja na hayo, kocha huyo ameonekana kufurahishwa kwa kurejea haraka kwa ligi kwani alikuwa akihofia viwango vya wachezaji kushuka.

"Sisi kama benchi la ufundi tumefurahi kwa sababu tulikuwa tunahofia viwango vya wachezaji kuporomoka, si wengi ambao wanaweza kujilinda na kuendelea kuwa fiti kwa kipindi chote hiki," alisema kocha huyo.

Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, JKT Tanzania ilimaliza ikiwa nafasi ya nane katika msimam ikiwa na pointi 19, ikicheza michezo 16, imeshinda minne, sare saba, imepoteza michezo mitano.

Wakati hayo yakiendelea, klabu hiyo imetangaza kumsajili straika, Ally Msengi akitokea Prisons.

Mchezaji huyo amesajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo la Danny Lyanga, aliyetimkia Mashujaa FC katika dirisha dogo la uhamisho lililofungwa Jumatano iliyopita.