TikTok yaacha kufanya kazi Marekani, siku chache kabla ya sheria mpya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:01 AM Jan 19 2025
TikTok yaacha kufanya kazi Marekani, siku chache kabla ya sheria mpya.
Picha: Mtandao
TikTok yaacha kufanya kazi Marekani, siku chache kabla ya sheria mpya.

Mtandao wa kijamii wa TikTok umesitisha huduma zake nchini Marekani, ikiwa ni saa chache kabla ya sheria mpya inayopiga marufuku matumizi ya mtandao huo kuanza kutumika rasmi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), marufuku hiyo imetokana na wasiwasi kuhusu uhusiano wa TikTok na Serikali ya China, huku tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa hatua hiyo ikiwa ni Januari 19, 2025.

Kauli za Viongozi

Rais wa Marekani, Joe Biden, ameeleza kuwa suala hilo sasa liko mikononi mwa mrithi wake, Donald Trump, ambaye anatarajiwa kuapishwa kesho Jumatatu.

Trump, akizungumza na NBC News jana, alisema kuna uwezekano wa kutoa msamaha wa siku 90 kwa TikTok ili kutoa muda zaidi wa kushughulikia masuala yanayohusiana na marufuku hiyo.

"Kuongezwa siku 90 ni jambo ambalo linaweza kutokea kwa sababu ni sahihi. Ikiwa nitaamua kufanya hivyo, labda nitatangaza kesho," amesema Trump.

Athari kwa Watumiaji

Watumiaji wa TikTok nchini Marekani wameripoti kuwa programu hiyo haipatikani tena kwenye maduka ya Apple na Google, na tovuti ya TikTok.com pia haionyeshi video yoyote.

Hatua hii inakuja wakati mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na China ukiendelea kuathiri mashirika mbalimbali, huku mustakabali wa TikTok nchini Marekani ukiwa bado haujabainika.