Wajumbe wammwagia sifa kedekede Wasira

By Augusta Njoji ,, Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 06:57 AM Jan 19 2025
Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamempongeza kuchaguliwa kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.

Wajumbe hao walitoa maoni yao baada ya kuahirishwa kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM jana jijini hapa.  

Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, alisema safu ya uongozi ndani ya CCM sasa imekamilika. 

Makamba alisema ndani ya miaka minne ilani ya CCM imetekelezeka kwa vitendo na hiyo ndio itakuwa siri ya ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu alisema Wasira amelea vijana wengi wa CCM, hivyo chama kimepata mtu mwajibikaji kiuzalendo, mwajibikaji, mwenye uwezo mkubwa wa kukisemea chama kwenye majukwaa.

“Ni mtu mwenye kujenga hoja, asiye mbinafsi, hivyo CCM tumelamba dume kwa kumpata Mzee Wasira, Gap la Kinana huenda watu walidhani tutampata nani wa kuziba nafasi hiyo hata hivyo tumepata wa kuziba pengo hilo,”alisema.

Mjumbe wa Utekelezaji Mkoa wa Dodoma, Dayana Ngurumo, alisema Wasira hana makundi, ana penda haki, anachapa kazi, anaijua kazi yake hivyo ataunganisha wana CCM hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Diwani wa Viti Maalum Chemba, Mwanaharusi Batu, alisema Wasira ni chaguo sahihi kwa kuwa wanajua kazi ambazo amewahi kuzifanya kwenye nyadhifa mbalimbali alizozitumikia.

Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi zilizomo kwenye ilani na kwamba hatua hiyo amewaachia deni la kuhakikisha anapata kura za kutosha kwenye uchaguzi mkuu. 

Mjumbe wa CCM kutoka Mkoa wa Morogoro, Frank Mgao, alimzungumzia Wasira kuwa ni mtu mzalendo, mkongwe wa siasa hivyo ataimarisha chama. 

Mjumbe wa CCM kutoka Mkoani Mwanza, Irene Jackson, alisema kuwa Wasira ni mvumilivu, anapenda umoja, haki, hivyo kilichotokea kupitishwa kwa jina lake maana yake ana sifa zote kushika wadhifa huo.

 â€śKwa kiasi kikubwa atakitetea chama, tumepata kiongozi ambaye ataleta mabadiliko na maendeleo ndani ya chama na wanachama wote,” alisema.