Shangwe zalipuka lilipotajwa jina la Stephen Wasira

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:15 AM Jan 19 2025
Shangwe zalipuka lilipotajwa jina la Stephen Wasira.
Picha:CCM
Shangwe zalipuka lilipotajwa jina la Stephen Wasira.

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu maalum wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waliibua shangwe na nderemo baada ya jina la mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira, kutangazwa kuwa mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara.

Akitaja jina la Wasira kwenye mkutano huo jana jijini hapa,  Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kada huyo ni mbobezi na yuko tayari kuvua shati kuikingia kifua CCM.

“Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum, katika kujaza nafasi hii, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa tulikaa tukaangalia wana CCM ambao wanaweza kujazia nafasi hii na tukampata mmoja ambaye ni mbobezi na yuko tayari kuvua shati kuikingia kifua CCM.  Naye  ni ndugu yetu, mzee wetu Stephen Wasira,” alisema Rais Samia.

Baada ya kutajwa jina hilo, ukumbi ulilipuka shangwe, nderemo na vigelegele kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo.  

Akisoma Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuhusu uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohamed Said Dimwa, alisema NEC ilimteua Wasira baada ya kujiridhisha juu ya tabia, mwenendo na sifa zake kwa muda wote wa uhai wake ndani ya CCM.

“Wasira ni muumini wa kweli wa siasa za chama chetu ya ujamaa na kujitegemea na anazingatia kikamilifu masharti ya wanachama, sifa na miiko ya kiongozi kama ilivyoainishwa katika Katiba ya CCM, na daima amekuwa mstari wa mbele kupigania na kulinda maslahi ya chama chetu pamoja na mshikamano wa kitaifa,”alisema.

Alieleza kuwa Wasira ni mkweli, mnyenyekevu, anapenda nchi yake na raia mwema wa Tanzania, ni muumini wa Muungano wa serikali mbili, mwana mapinduzi anayependa maendeleo ya nchi yake, haki na usawa na kuchukia rushwa kwa vitendo sio kwa maneno.

“Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inamshukuru kwa dhati Makamu Mwenyekiti mstaafu Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, kwa uongozi na utumishi wake uliotukuka katika chama chetu na taifa kwa ujumla, yeye pamoja na viongozi wengine wastaafu wa CCM wataendelea kuwa hazina ya chama na mlezi wa viongozi wa sasa na baadae wa CCM,” alisema.

Alisema daima wataendelea kumkumbuka na kumuenzi kama mwalimu na mlezi wao wa kisiasa, mfano mzuri wa kuigwa katika kujitolea na kuwatumikia wananchi kwa ujumla upendo, uadilifu na uaminifu.