Mbowe aahidi mambo saba, Lissu azidi kuwavutia wenyeviti mikoa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:27 AM Jan 20 2025
Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Picha:Mtandao
Freeman Mbowe na Tundu Lissu.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanya usaili kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kabla ya kwenda kupigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utakaofanyika kesho Dar es Salaam.

Wagombea hao ni wa nafasi za Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar pamoja na wagombea wa ujumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.

Baraza Kuu la chama hicho ndilo limefanya usaili wa wagombea hao. Wagombea wa nafasi ya mwenyekiti ambao walisailiwa jana ni Freeman Mbowe (anayetetea nafasi yake) na ambaye jana alitangaza vipaumbele vyake; Tundu Lissu (Makamu Mwenyekiti Bara) na Charles Odero.

Katika nafasi ya wagombea wa nafasi za Makamu Mwenyekiti kwa Tanzania Bara ni Ezekia Wenje (Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria) na John Heche.

Wengine ambao walifanyiwa usaili hiyo jana ni wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

AHADI YA MBOWE

Wakati huo Mbowe jana alisambaza vipaumbele vyake ambavyo anavyotarajia kuvitekeleza ikiwa atachaguliwa tena kuendelea kuongoza chama hicho.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuunda tume anayoita ya ukweli na upatanisho ndani ya chama hicho ili kutibu majeraha ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho na kuhakikisha CHADEMA yote inarudi katika umoja na mshikamano chini ya kaulimbiu yake ya ‘Stronger Together’.

Kipaumbele kingine, alisema ni kuboresha, kutanua na kuendeleza utekelezaji programu muhimu za ujenzi na ustawi wa chama na wanachama hususani kuondoa dosari na kuendeleza programu GF na CHADEMA Digital.

Kingine ni kuimarisha CHADEMA Family kwa kuanzisha mfuko rasmi wa kuwezesha wana-CHADEMA kusaidiana na kunyanyuana kiuchumi na kijamii (CHADEMA Family Fund) utakaochangiwa na kusimamiwa na wanachama wenyewe chini ya uangalizi wa chama.

Pia kutanua huduma ya msaada wa kisheria ya ndani ya chama ili kuondoa hofu na kuongeza ujasiri kwa wana-CHADEMA na wananchi katika kupigania na kupata haki zao.

Kipaumbele kingine, Mbowe alisema ni kuamsha vuguvugu kali la madai ya Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na sheria bora za uchaguzi, kwa kutumia nguvu ya umma na kwa kujenga uhusiano na ushirikiano na wadau mbalimbali wa siasa na demokrasia wa ndani na nje ya nchi katika kushinikiza mageuzi chini ya kaulimbiu yao ya ‘no reforms, no elections’.

Kadhalika, alisema ataanzisha programu kabambe na endelevu ya kuandaa na kuwawezesha wagombea wa chama hicho kushinda chaguzi, jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kugharimia sehemu kubwa ya kampeni na ulinzi wa kura katika ngazi zote kwa kuzipatia kipaumbele kikuu.

Mbowe alisema ataanzisha pia programu ya kimkakati na endelevu ya kutoa elimu ya uraia na elimu ya siasa, ili kutengeneza jamii kubwa ya watanzania wenye uelewa mkubwa na ujasiri wa kutosha katika kupigania haki zao za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Uchaguzi wa viongozi hao wa kitaifa wa chama cha CHADEMA utafanyika kesho katika ukumbi wa Mliman City, Dar es Salaam.

WENYEVITI NA LISSU

Jana wenyeviti wa mikoa 21 na makatibu wao walikusanyika katika moja ya hoteli zilizoko karibu na Kijiji cha Makumbusho, wilayani Kinondoni na kutoa tamko la pamoja la kumuunga mkono Lissu.