Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) limezindua rasmi safari zake za kila siku kati ya Johannesburg, Afrika Kusini, na Dar es Salaam, Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya mataifa haya mawili yenye ushawishi mkubwa barani Afrika.
Katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa SAA, Profesa John Lamola, alisema: "Njia hii ya anga si tu hatua muhimu kwa SAA katika kuunganisha Johannesburg na Dar es Salaam, bali pia inatangaza daraja linalounganisha mataifa mawili yenye nguvu kiuchumi. Inaleta pamoja viwanda, jumuiya, na rasilimali, huku ikifungua milango ya fursa mpya za biashara, uwekezaji, na maendeleo kwa watu wa Afrika Kusini na Tanzania."
Dar es Salaam, mji mkubwa zaidi Afrika Mashariki, ni kitovu muhimu cha kiuchumi na lango kuu la biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda huu. Aidha, jiji hili linahudumu kama lango la vivutio maarufu vya utalii, likiwemo Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na visiwa vya Zanzibar.
Afrika Kusini ni mwekezaji mkubwa nchini Tanzania, hasa katika sekta za kilimo, madini, kemikali, na mashine. Uzinduzi wa safari hizi unatarajiwa kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.
Profesa Lamola aliongeza kuwa uzinduzi huu ni sehemu ya mpango wa SAA wa kuimarisha mtandao wake wa kikanda barani Afrika.
"Mtandao wa kikanda wa SAA umeibuka kama kitovu muhimu cha mapato yetu, huku ukichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi ya Afrika Kusini. Uhusiano huu wa kikanda ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa kibiashara na kiuchumi wa kanda nzima," alisema.
Ratiba ya Ndege
Safari za ndege za kila siku zitaondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo, Johannesburg, saa 4:00 usiku (SAST) na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa 8:30 alfajiri (EAT). Safari ya kurudi kutoka Dar es Salaam itaondoka saa 11:10 alfajiri (EAT) na kufika Johannesburg saa 1:55 asubuhi (SAST).
Ratiba hii imelenga kuhudumia abiria wa ndani na wale wanaoendelea na safari zao kupitia mtandao wa kikanda wa SAA.
Mbali na safari za Dar es Salaam, SAA imeongeza safari zake kwenye miji mingine kama Harare (Zimbabwe) na Lusaka (Zambia), na kufikia safari 12 kwa wiki. Vilevile, safari za Lagos (Nigeria) na Accra (Ghana) zimeongezwa hadi mara nne kwa wiki, huku Kinshasa na Lubumbashi (DRC) zikihudumiwa mara tano kwa wiki.
Pia, safari za kimataifa kwenda Perth, Australia, zimeongezwa hadi mara tano kwa wiki, hatua inayoonyesha dhamira ya SAA ya kukuza mtandao wake wa kimataifa.
Kwa uzinduzi wa safari hizi mpya, SAA inaendelea kuwa kiunganishi muhimu barani Afrika, ikisaidia kukuza uchumi na kuimarisha uhusiano wa kijamii na kiutamaduni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED