Wajipanga kuleta mapinduzi ya kilimo

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:08 AM Apr 27 2024
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Obadia Nyagiro
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Obadia Nyagiro

WADAU wa kilimo ikolojia hai wamejipanga kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo nchini kwa kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2024/25 kwa ajili ya utekelezaji vipaumbele vya mkakati wa kitaifa wa kilimo hai wa ikolojia wa 2023-2030 (NEOAS).

Akizungumza juzi kwenye kikao hicho kilichoratibiwa na Mwavuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Obadia Nyagiro, alisema kilimo hicho ni muhimu kwa watanzania kwa kuwa kitaleta tija kiuchumi, kulinda afya za walaji, afya ya udongo na kuongeza kipato.

Alisema mkakati huo unatokana na Sera ya Kilimo kuelekeza masuala ya kuweka mfumo wa uzalishaji, upatikanaji wa masoko na kutambua bidhaa za kilimo hai.

Nyagiro alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha uandaaji wa mpango huo kwa kuwa ni muhimu wadau kushiriki katika kilimo himilivu na endelevu kwa mazingira na afya ili kuleta tija kwenye sekta ya kilimo.

Alizitaka asasi za kiraia na sekta binafsi kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika kilimo hicho kwa kuwa kina tija kubwa.

“Nihimize sekta binafsi na asasi za kiraia mpitie na kuona fursa ya kuwekeza katika eneo hili kwa kuwa tija yake ni kubwa ikiwamo kuongezeka kwa mapato, mkipitia nchi nyingine mtaona waliowekeza kwenye kilimo hiki na tija yake na ni muhimu  mipango yetu izingatie kilimo himilivu kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa TOAM, Dk. Mwatima Juma, alisema kilimo hicho kinalenga kuwa na uzalishaji wa kutosheleza kulinda afya na udongo kwa kuondokana na matumizi ya kemikali.

“Kilimo cha kutumia kemikali kilianza miaka 100 iliyopita baada ya kuisha kwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia ambapo utengenezaji wa mbolea za kemikali, viuatilifu vya kemikali ilionekana itatusaidia kuzalisha chakula zaidi.

“Tulihamasika kuwa kutumika kemikali ndo ukisasa na kwa bahati mbaya tuliacha kilimo chetu cha asili ambacho mtu alikuwa akilima kahawa ndani yake ana kunde,maharage, mtama vyote vinazalishika vizuri na ana ng’ombe anatupia mbolea shambani kwake,” alisema. 

Aliongezak uwa: “Tukahamasisha tuwe na mashamba makubwa tulime zao moja, tupulize dawa miaka imekwenda na tulipofika mimi binafsi nasema tuwaombe radhi wakulima kwa maeneo tuliyowapeleka hasa wakulima wadogo hapafai, kuna aina ya ukulima wanaweza kulima bila kupunguza uzalishaji, bila kupata shida kwenye chakula na kuuza kwenye masoko ya ndani na nje.

Alibainisha kuwa kilimo hicho kitasaidia watanzania kuondokana na maradhi mbalimbali ikiwamo uzazi, saratani kwa kuwa yanatokana na matumizi ya kemikali kwenye kilimo.

Naye Paul Holmbeck  kutoka Shirika la  Biovision Foundation akizungumzia mataifa mengine namna yanavyotekeleza kilimo hicho, alisema wanasayansi na mashirika ya kimataifa ya masuala ya kilimo yanahimiza kilimo hicho kwa usalama wa chakula na kuna tija kiuchumi ambapo serikali za nchi ambazo zinatekeleza kilimo hicho zinaweka malengo yake.