WADAU wa Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto nchini wamesema kuzidi kwa hali ya udumavu wa akili pamoja na utapiamlo kwa watoto nchini kunahitaji ushirikishwaji na elimu ya mara kwa mara kwa wazazi ili kutambaua namna ya kuchangamsha watoto pamoja na vyakula gani na muda gani wapatiwe kuimarisha lishe zao.
Hayo yamebainishwa Novemba 9, 2024 na Mkurugenzi wa Shirika ya Tanzania Early Childhood Education and Care (TECEC), Joel Elphas wakati wa semina kwa wazazi jijini Mwanza iliyofanyika katika kituo cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto cha shirika hilo.
“Katika kupambana na hali hii ya udumavu wa akili ni lazima mzazi awe sehemu ya kumuandaa mtoto kuanzia miaka sifuri mpaka nane akimfanyisha vitu vya uchangamshi, kumtengenezea zana mbalimbai za michezo zitakazo msaidia kumudu K tatu (kuoma, kuandika na kuhesabu) kabla hajaanza masomo,” amesema Joel.
Kuhusu utapiamlo, Joel amesema si kwamba wazazi hawana vyakula vyenye lishe kwaajili ya watoto wao bali hali ya mazoea na kutokufuata mlo kamili ndicho chanzo cha tatizo hilo.
“Wazazi wanatakiwa kutambua namna ya kuandaa vyakula vinavopatikana katika mazingira yao ili kutengeneza lishe bora kwa watoto wao na hii ndiyo elimu ya msingi tunayoitoa katika kituo chetu pamoja na kwenye mikutano mbalimbali ya lishe. Vilevile tunacho kituo cha kutengeneza unga wenye virutubisho kwaajili ya watoto,” amesema Joel.
Awali akitoa elimu kwa wazazi, mtaalam wa malezi na makuzi ya mtoto, Magdalena Tenethain amewataka wazazi kuwekeza zaidi kwa watoto wenye umri wa miaka sifuri mpaka nane ili kuwaandalia msingi bora na imara wa maisha yao ya baadaye.
“Yote tunayoyaona kwa sasa ni kutokana na kuwa wazazi tumesahau wajibu wetu kwa kujiwekeza zaidi katika utafutaji na kusahau jukumu letu muhimu la malezi kwa mtoto,”amesema Magdalena.
Ofisa Maendeleo Mkoa wa Mwanza, Janeth Shishila amesema licha ya mapambano yanayofanywa na serikali kupitia wizara mbalimballi ikiwemo ofisi ya waziri mkuu kukabilia na tatizo hilo bado ipo haja ya mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia katika kutokomeza janga hilo kwa watoto.
“Shirika hili limekuwa mfano kwa kujenga kituo kwaajili ya malezi na makuzi ya mtoto kikitoa malezi kwa watoto, elimu kwa wazazi na kujitolea kurytumisha unga ili kuhakikisha watoto wanakuwa na lishe bora na utimamu wa akili wote tuige mifano hii muhimu kwani serikali haiwezi kufanya kila kitu,”amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED