TIC, TRA kuwakutanisha wawekezaji wa nje

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:06 PM Oct 28 2024
Mkurugenzi Mhamasishaji TIC, John Mnali, kulia akizungumza na waandishi leo.
Picha Maulid Mmbaga
Mkurugenzi Mhamasishaji TIC, John Mnali, kulia akizungumza na waandishi leo.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameandaa mkutano maalumu utakaowakutanisha wawekezaji wa nje kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kikodi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mhamasishaji TIC, John Mnali, amesema katika mkutano huo utakaofanyika Oktoba 31, mwaka huu pia watapata fursa ya kuwasilisha taarifa za maboresho mbalimbali ya sera za uwekezaji na kikodi.

Amesema kutokana na kwamba TIC inatoa huduma zinazojumuisha taasisi mbalimbali, pia wakuu wa taasisi hizo watashiriki katika mkutano huo, utakaofanyika mkoani Dar es Salaam.

"Katika mkutano huo itatolewa taarifa ya maboresho mbalimbali ambayo kimsingi yanasaidia uwekezaji mzuri, lakini itakuwa ni fursa nzuri kwa wawekezaji wa nje kutoa madukuduku yao na kupatiwa ufafanuzi endapo ukihitajika," amesema Mnali.

Ameongeza kuwa TIC kwa kushirikiana na TRA watakuwa na wataalamu kutoka kila idara na taasisi zingine za serikali ambazo zina uwakilishi kwenye eneo la utoaji huduma kwa wawekezaji, ambao watatoa ufafanuzi kutoka katika idara zao pale ambako utahitajika.

Meneja Elimu kwa Mlipakodi TRA, Paul Walalaze, amesema makusanyo ya kodi bila uwekezaji hawawezi kusonga mbele, huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuweka mazingira radiki ya kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.