RC Macha akabidhi gari jipya kwa RUWASA

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:05 PM Oct 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia) akikata utepe kukabidhi gari jipya kwa RUWASA (kushoto) ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela.
Picha: Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia) akikata utepe kukabidhi gari jipya kwa RUWASA (kushoto) ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amekabidhi gari jipya kwa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA)Mkoa wa Shinyanga, huku akisisitiza litumike kwa malengo kusudiwa pamoja na kutunzwa.

Hafla ya kukabidhi gari hilo lenye namba STN 2943 imefanyika leo Oktoba 28,2024 katika Ofisi ya mkuu wa mkoa huyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na watumishi wa RUWASA.

Macha akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, amewataka RUWASA kwamba walitumie kwa malengo yaliyokusidiwa kwa shughuli za kiserikali, ikiwamo kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maji ambayo inatekelezwa kwa wananchi.

“Tunampongeza Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa vitendea kazi katika sekta mbalimbali na leo hapa Shinyanga tunakabidhi gari jipya kabisa kwa RUWASA ili kuongeza ufanisi wa utendaji wao kazi na kuwahudumia wananchi kupata huduma ya majisafi na salama na kumtua ndoo kichwani mwanamke,” amesema Macha.

 Amesisitiza pia, gari hilo linatunzwa kwa maslahi mapana ya Serikali ili lidumu muda mrefu,pamoja na kufanyiwa “service” mara kwa mara ili siharibike mapema.

 Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela, amemshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha ofisi yake kupata kitendea kazi, ambacho kinakwenda kuongeza ufanisi na uboreshaji wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, pamoja na kusimamia vyema miradi ya maji ambayo inatekelezwa mkoani humo, ili iwe na kiwango chenye ubora na kukamilika kwa wakati.