Naibu Waziri awaomba viongozi wa dini wasaidie kukabili kipindupindu, Mpox

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 11:26 AM Oct 28 2024
news
Picha:Mtandao
NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel

NAIBU Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amewaomba viongozi wa dini nchini, kusaidia serikali kutoa elimu sahihi ya kuepuka magonjwa ya mlipuko kama Mpox, kipindupindu na Marbug.

Dk. Mollel alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, kwenye mkutano na viongozi wa dini kuhusu tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko na suala la bima ya Afya kwa Wote.

Alisema viongozi hao wana wajibu wa kiroho kusaidia kuhakikisha wanalinda jamii na maradhi yanayoepukika kwa kutumia nyumba zao za ibada.

"Tunazungumza na ninyi kwa niaba ya waumini; viongozi wa dini kote nchini isaidieni serikali kutoa elimu sahihi ya kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama Mpox, kipindupindu na Marbug.

"Wakati tunafuatilia wasilisho, tumeona ramani ya Tanzania ikiwa nyeupe lakini wenzetu wanaotuzunguka wameshapata visa vya baadhi ya magonjwa ya mlipuko. Sasa niwaombe mwende mkazungumze na wanajamii, ili ramani ya Tanzania izidi kubaki nyeupe," alisema Dk. Mollel.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. John Jingu, alisema ipo haja ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, ili wananchi ambao ni waumini katika nyumba za ibada wawe salama na kuendelea na majukumu yao.

"Tumekubaliana tunatoka hapa tukiwa na nia moja, tunakwenda kuwahimiza waumini wetu, lakini pia na sisi wenyewe kuwa usafi ndio kila kitu, baadhi ya mila na desturi zetu zinazokuwa hatarishi, tuziepuke na sisi tuwajibike.

"Lazima tuhakikishe tunaendelea kuwa salama na mwisho wa siku nchi yetu kwa ujumla itakuwa salama," alisema Dk. Jingu.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Ibrahim Hussein, alipongeza serikali kwa kutumia majukwaa ya dini kuendelea kufikisha elimu ya afya kwa umma na kuahidi kwenda kuwahimiza waumini dhidi ya magonjwa hatarishi ya mlipuko.

"Hatua ya serikali kukutana na wadau mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini, ni nzuri sana na inafaa iendelee kwa sababu viongozi wa dini wanawafikia wananchi wengi sana. Hivyo, wakipata elimu kama hii itasaidia kuepuka magonjwa mbalimbali," alisema.