Pwani yalenga kupata asilimia 99 ya korosho daraja la kwanza msimu huu

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 12:44 PM Oct 28 2024
Pwani yalenga kupata asilimia 99 ya korosho daraja la kwanza msimu huu
Picha:Mpigapicha Wetu
Pwani yalenga kupata asilimia 99 ya korosho daraja la kwanza msimu huu

Wadau wa korosho katika Mkoa wa Pwani wamejipanga kuhakikisha msimu huu wa korosho wanazalisha asilimia 99 ya korosho za daraja la kwanza, hatua inayolenga kuboresha ubora na bei sokoni.

Meneja wa CORRECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mnada wa pili wa korosho uliofanyika Kingombera, wilayani Mkuranga.

"Asilimia 99 ya korosho tunataka iwe daraja la kwanza na inatokea Mkoa wa Pwani," alisema Mantawela, akisisitiza lengo la kuhakikisha Pwani inaendelea kuwa kinara katika uzalishaji wa korosho bora nchini.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Mkoa wa Pwani umekuwa ukijipambanua kwa uzalishaji wa korosho zenye ubora wa hali ya juu, hatua iliyopelekea kufanikisha mnada wa tani tisa za korosho katika minada miwili iliyofanyika hadi sasa. 

Aliongeza kuwa korosho daraja la kwanza zimeuzwa kwa zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo, huku daraja la pili likiuzwa kwa zaidi ya shilingi 2,000 kwa kilo, ikionesha jinsi ubora unavyohusiana na bei nzuri sokoni.

Mantawela aliwahimiza wakulima kuzingatia ubora na kuhakikisha korosho wanazopeleka mnadani zinakidhi viwango vya daraja la kwanza, kwani hali ya hewa kwa sasa ni nzuri kwa kilimo bora. 

Pia alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya wakulima kuwahamasisha wakulima kufuata masharti yanayowekwa sokoni na kuzingatia mikataba yao ili kupata malipo ya haki.