e-GA yatakiwa kuendeleza ushirikiano na e-GAZ

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:08 PM Oct 28 2024
e-GA yatakiwa kuendeleza ushirikiano na e-GAZ
Picha:Mpigapicha Wetu
e-GA yatakiwa kuendeleza ushirikiano na e-GAZ

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GAZ) ili kusaidia maendeleo ya TEHAMA visiwani Zanzibar.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Machano Othman Said wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea Makao Makuu ya e-GA Mtumba jijini Dodoma na kupokea taarifa ya utekelezaji wa afua mbalimbali za serikali Mtandao kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba.

Mwenyekiti huyo amesema Taasisi hizo mbili ni muhimu katika kukuza Uchumi wa nchi,hivyo ushirikino wa karibu ni muhimu ili kuweka usawa wa matumizi ya Tehama katika taasisi za umma kote bara na visiwani.

“Ndugu Ndomba tunaomba utusaidie kwenye hili, e-GAZ bado ni changa,tunahitaji Zanzibar nayo iingie kwenye matumizi ya kidigiti,tunahitaji kufika hadi kwa mashea wote watumie mifumo ya Tehama katika shughuli zao za kila siku,” ameeleza

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi  Ndomba, ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanziba (eGAZ) ili kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika kote Bara na Visiwani ili kuboresha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi.