Mradi wa HEET kunufaisha wanafunzi mikoa ya pembezoni

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 01:23 PM Oct 28 2024
Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia WB, (wa tatu kushoto) Profesa Roberta Malee, akizungumza na wataalam wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo ya Chuo cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Picha: Grace Mwakalinga
Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia WB, (wa tatu kushoto) Profesa Roberta Malee, akizungumza na wataalam wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo ya Chuo cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

KABLA ya kuanzishwa kwa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi Tanzania (HEET), vikwazo vya upatikanaji wa elimu ya juu katika mikoa ya pembezoni kama vile Mara, Kigoma na Katavi zilikuwa kubwa, wanafunzi wengi walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata masomo mikoa mingine.

Lakini sasa, Chuo cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Kambarage Nyerere, kilichopo Butiama, kimepokea ufadhili wa shilingi bilioni 102.5, ambazo zitatumiwa kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za masomo kwa wanafunzi wa mikoa hiyo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Bernard Mellau, amesema kuwa kati ya fedha hizo kiasi cha sh. bilioni 16 zinatumiwa kujenga majengo sita katika kampasi mpya mkoani  Tabora ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha watanzania wote wanapata elimu ya juu katika mazingira bora.

Amesema kampasi kuu ya Butiama, ujenzi wa majengo 16 umeanza, na hatua za mradi zimefikia  kwa asilimia 41, alidai ni mwanzo wa mabadiliko makubwa  kwa sababu  wanafunzi wa maeneo ya mbali wataweza kupata elimu ya juu karibu na makazi yao, hivyo kuwapatia nafasi za kujenga maisha bora na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Mradi huu unatarajiwa kuleta sura mpya katika elimu ya juu nchini, kwa sababu unahamasisha  vijana wengi kujiunga na vyuo na kujiandaa kwa ajira na kazi za ubunifu zinazohitajika katika soko la ajira,” amesema Prof Mellau.

Amesema Chuo hicho kina  uwezo wa kuhudumia wanafunzi 6,000 ifikapo mwaka 2025, kampasi kuu ya Butiama ikipokea wanafunzi 4,500 na kampasi ya Tabora ikihudumia wanafunzi 1,500.

1

“Tuna matumaini kuwa mradi huu utawapatia wanafunzi mikoa ya pembezoni fursa bora zaidi za elimu, na kwa sasa tunashirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu, Benki ya Dunia, taasisi za elimu na vyuo vikuu vingine ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” ameongeza Profesa Mellau.

Amedai  kuwa chuo hicho tayari kina wanafunzi 71 waliosajiliwa, kati ya nafasi 150 zilizotengewa, lakini alieleza kikwazo muitiko kujiunga na chuo hicho ni mdogo kwa sababu baadhi ya wanafunzi wanaonekana kuvutiwa zaidi na vyuo vingine vyenye majina makubwa.

Akizungumza maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Peter Msofe, amesema kuwa mradi wa HEET unatekelezwa kwa gharama ya dola za kimarekani  milioni 425  sawa na  takribani sh. trilioni moja za kitanzania katika taasisi 23 za elimu ya juu nchini.

Amesisitiza kuwa, licha ya mradi huo kuwa na lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi, unalenga pia kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini.

“Utaona mahali tulipo mwaka jana kulikuwa ni pori, lakini sasa tayari kuna majengo, tunaamini mwakani tutaanza kuona wanafunzi wakisoma hapa, hii ni nia ya serikali kutumia elimu ya juu kama chachu ya kuleta maendeleo nchini,” amesema Msofe. 

Mhandisi Mshauri Mkazi wa ujenzi wa mradi huo, Silvester Francis, ameeleza kwamba mradi ulianza rasmi mwezi Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Mei 2025.

2

Amesema  kwa sasa, mradi huo upo katika hatua mbalimbali za ujenzi, awamu ya kwanza inajumuisha majengo saba kwa gharama ya sh bilioni 20.5 ya pili ina majengo manne, inagharimu bilioni 16.9, aidha, kuna majengo mawili ya utawala na maktaba yanayogharimu bilioni 21.

Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia, Profesa Roberta Malee, alipongeza kasi ya ujenzi na kiwango cha ubora kinachozingatiwa, alieleza kufurahishwa  kuona ujenzi ukiendelea kwa kasi na kwa viwango vinavyohitajika, alisema  hatua hiyo imeonyesha azma  ya kuboresha miondombinu ya  elimu ya juu nchini.

Mtaalam Mwandamizi wa Elimu na Kiongozi Mwenza wa Mradi wa HEET, Mkaiga Kaboko, amesema  mradi huo utachochea uchumi kwa kuzalisha wataalam ambao wataajiriwa katika sekta mbalimbali.

Amesema elimu ya juu yenye ubora huchangia katika kuzalisha ajira na kuimarisha utafiti ambao utasaidia maendeleo ya kiuchumi nchini alidai hiyo ni juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa sekta ya elimu ya juu inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi.

3

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha gharama za ujenzi zinaendana na bajeti, Kaboko alifafanua kuwa wameanzisha utafiti wa gharama ili kupata mlinganisho wa gharama za miradi mingine na kuhakikisha wakandarasi wanazingatia mikataba kwa usahihi, alisema hatua hiyo  zinakusudia kuzuia ongezeko la gharama kutokana na kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi, na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa gharama iliyopangwa.

Mradi wa HEET unaendelea kutoa matumaini mapya kwa watanzania, hususani vijana wa mikoa ya pembezoni, kwa kuweka msingi imara wa elimu na maendeleo ya kiuchumi, na kuandaa jamii kwa ajili ya ustawi endelevu.