Tembo kuharibu nyumba za wananchi Ikungi, Waziri Chana atinga

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:20 AM Oct 28 2024
Tembo kuharibu nyumba za wananchi Ikungi, Waziri Chana atinga
Picha:Thobias Mwanakatwe
Tembo kuharibu nyumba za wananchi Ikungi, Waziri Chana atinga

SIKU mbili baada ya wananchi wa kijiji cha Mkiwa wilayani Ikungi mkoani Singida kufunga barabara kushinikiza serikali iwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu baada ya tembo kuharibu nyumba zao, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi,Dk. Pindi Chana,amewasili katika wilaya hiyo kuzungumza na viongozi na wananchi.

Waziri Chana kabla ya kuzungumza na wanakijiji  amefanya kikao cha ndani cha viongozi na kupewa taarifa kuwa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu yameongezeka katika Mkoa wa Singida ambapo katika kipindi cha Januari hadi Julai 2024 kumetokea matukio 162 na halmashauri zinazoongoza kwa matukio ni Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Manyoni na Ikungi.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kanda ya kati, Herman  Nyanda, amemweleza Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa pia katika kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Disemba 2023 kulitokea matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu 359 katika Mkoa wa Singida.

Nyanda amesema changamoto zinazosababisha kutokea kwa matukio hayo ni kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika shoroba za wanyamapori na kutozingatia mipango ya matumizi ya ardhi ambapo vijiji vingi vyenye mipango havizingatii kutenga maeneo ya korido ya wanyamapori.