TCRA: Huduma za kidigitali zinazidi kuwafikia wengi nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:20 AM Oct 28 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari.

SEKTA ya Mawasiliano Tanzania, imeendelea kuimarika ndani ya miezi mitatu kutokana na kuenea huduma zinazotumia teknolojia za kidigitali katika maeneo mengi nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari, aliyasema hayo jana, wakati akizungumzia ukuaji wa mawasiliano nchini. 

Alisema kuenea kwa teknolojia na vifaa vya watumiaji miongoni mwa watu kuliongezeka kwa kati ya pointi moja na tatu kati ya Juni na Septemba, 2024. 

"Huduma zinazowezeshwa na teknolojia za juu zaidi pia zimeongeza kasi ya intaneti, zimewezesha mitandao kuimarika na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Teknolojia zimeongeza ubora wa huduma. 

"Teknolojia za simu za mkononi uzao wa tatu (3G) zimezidi kuenea kwa watu, kutoka asilimia 89 hadi 90.1. uzao wa nne (4G) umeenea zaidi kutoka asilimia  83 hadi 84.9 na wa tano (5G) kutoka asilimia 15 hadi 18," alisema. 

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kijiografia, 4G imeenea asilimia 73.6 kutoka asilimia 73 na 4G kwa asilimia 70.2 kutoka asilimia 69. Uzao wa tano kijiografia umeenea asilimia 2.2 Septemba 2024 kutoka asilimia mbili Juni mwaka huu. 

"Teknolojia hizi zinawezesha huduma za maongezi, ujumbe mfupi (meseji) na intaneti. Teknolojia ya 5G ambayo iliingia Tanzania mara ya kwanza mwaka 2022, ina kasi kubwa ya intaneti, inapunguza ucheleweshaji kusafirisha data na inaunganisha watumiaji na mitandao kwa ufanisi zaidi," alisema.

Dk. Jabir alisema taarifa hiyo imeeleza kwamba simu zenye uwezo mkubwa au simu janja. zimeenea miongoni mwa watu, kwa asilimia 33.85 kutoka asilimia 31.5 Juni 2024. 

"Simu janja zina programu tumizi changamani zaidi na zinawezesha intaneti ya kasi. Watumiaji intaneti Tanzania wameongezeka kwa  asilimia tano kati ya Julai na Septemba 2024 kutoka milioni 39.3 hadi 41.4," alisema.

 Alisema watumiaji wanakokotolewa kutokana na laini za siku zilizotumika kutoa huduma ya intaneti ndani ya miezi mitatu iliyotangulia kwa kutumia teknolojia yoyote ile. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, huduma za intaneti zinapatikana zaidi  kupitia vifaa vya mkononi na visivyo na waya. Taarifa inaonesha asilimia 99.7 ya watumiaji intaneti walipitia  teknolojia za vifaa vya mkononi.

 "Matumizi ya data yameongezeka kutoka wastani wa megabaiti  (MB) 4.647 kwa mtumiaji Juni mwaka huu hadi MB 4.855 Septemba, 2024," alisema.

Aliongeza kuwa wastani wa kasi ya kupakia data kwa watumiaji vifaa vya mkononi vinavyowezesha intaneti ya kasi, unaopimwa kwa megabaiti moja kwa sekunde (Mbps), uliongezeka kutoka Mbps 11.4 Juni hadi 13.3 Septemba, 2024.